Je, kujiondoa kwa Biden kunamaanisha nini kwa Harris, Democrats na Trump?

.

Chanzo cha picha, Reuters

Maelezo ya picha, Kamala Harris kwenye ukumbi wa jiji huko Pennsylvania

Joe Biden amebadilisha uchaguzi wa Marekani. Baada ya kusisitiza kwa wiki kadhaa kwamba angesalia kuwa mgombea wa kiti cha urais kupitia chama cha Democrats, amekubali shinikizo na kujiondoa katika kinyang’anyiro hicho.

Je hatua yake ina maana gani kwa Makamu wa Rais Kamala Harris, kwa Wanademokrats na upana zaidi kwa Donald Trump?.

Je, Kamala Harris ndio chaguo lililosalia kwa Democrats?

Matarajio ya Kamala Harris kuwa mteule wa chama cha Democrats yamepata msukumo mkubwa na uungaji mkono wa Joe Biden.

Alimuunga mkono kikamilifu, akitaja uamuzi wake wa kumfanya makamu wake wa rais miaka minne iliyopita kuwa bora zaidi aliyowahi kufanya.

Alijibu kwa kusema kuwa ameheshimu kupata uungwaji mkono wake na atafanya kila liwezekanalo kushinda uteuzi huo.

Inawezekana kwamba Wanademokrats wengi watafuata mwongozo wa rais na kuwa nyuma ya makamu wa rais ili kuepusha kutokuwa na uhakika chini ya mwezi mmoja kutoka kwa kongamano la Democrats

Kuna sababu za kiutendaji na kisiasa za kufanya hivyo.

Anafuata katika safu ya katiba ya urithi.

Maoni ya kumpuuza mwanamke wa kwanza mweusi kwenye tikiti ya urais itakuwa mbaya kwa chama.

Pia ataweza kupata mara moja takriban dola milioni 100 za fedha ambazo kampeni imechangisha kufikia sasa.

Lakini pia kuna hatari.

Uchunguzi wa maoni ya umma unaonyesha kwamba umaarufu wake uko sawa na ule wa rais Biden akilinganisha na umaarufu wa Donald Trump.

.

Chanzo cha picha, Reuters

Maelezo ya picha, Kamala na Joe Biden

Pili ni kwamba Harris amekuwa mara nyengine na wakati mgumu kama makamu wa rais.

Mapema katika utawala wa Biden, alipewa jukumu la kushughulikia sababu kuu za mzozo wa wahamiaji kwenye mpaka wa Marekani na Mexico.

Hiyo ni changamoto ya kutisha, na makosa kadhaa na taarifa potofu zilimfanya akosolewe.

Pia amekuwa mhusika mkuu wa utawala kuhusu haki za uavyaji mimba, mada ambayo ameshughulikia kwa ufanisi zaidi.

Lakini maoni hayo ya kwanza yamemuharibia sifa.

Hatimaye, na pengine muhimu zaidi, Harris tayari amewania wadhifa wa kitaifa – azma yake ya 2020 ya uteuzi wa urais wa Democrats – ambapo alianguka vibaya.

Umaarufu wake ulipopanda mapema, mchanganyiko wa mahojiano yasiyoeleweka, ukosefu wa maono yaliyofafanuliwa wazi na kampeni iliyosimamiwa vibaya ilimfanya aache kuwania hata kabla ya kura za awali za mchujo.

Kumchagua Harris ni hatari kwa Wanademokrats, lakini kwa wakati huu hakuna chaguo salama huku uwezekano wa ushindi wa Donald Trump – ukiendelea kuongezeka

Kongamano la Democrats linaweza kuwa na msukosuko

Katika kipindi cha nusu karne iliyopita, makongamano ya kisiasa yamegeuzwa kuwa maeneo ya kupoteza wakati na kuchosha.

Huku kila dakika ikiandikwa kuimarisha kipindi cha televisheni, yamekuwa yakitumika kama matangazo ya wagombea wa urais.

Kongamano la wiki iliyopita la chama cha Republican kwa hakika lilikuwa hivyo hivyo – hotuba ndefu ya Donald Trump, ya kukubali uteuzi wakati mwengine iliwachosha wengi.

Kongamano la Democrats la mwezi ujao hatahivyo linatarajiwa kubadilika na kuwa tofauti sana.

Hati yoyote ambayo chama na kampeni ya Biden ilikuwa ikifanyia kazi sasa imetupiliwa mbali.

Hata iwapo chama kitamuunga mkono bi. Harris, itakuwa vigumu kupanga – na kudhibiti – jinsi mambo yanavyotokea kwenye mkutano huo.

Na ikiwa Harris hatafanikiwa kukiunganisha chama, kongamano hilo linaweza kugeuka na kuwa la kisiasa kwa wote, huku wagombea mbalimbali wakiwania uteuzi mbele ya kamera na milango iliyofungwa.

Unaweza kuwa ukumbi wa michezo wa kisiasa unaovutia, ambao hautabiriki, kwa njia ambayo umma wa Marekani haujawahi kushuhudia.

Kwa Republican ni nguvu dhidi ya udhaifu

Kongamano la mwaka huu la chama cha Republican lilikuwa mashine iliyorekebishwa kwa uangalifu, likikuza ajenda maarufu zaidi za chama na kulenga ukosoaji kwa mtu mmoja, Rais Joe Biden.

Sasa imetokea kwamba Republicans walikuwa wanalenga mtu tofauti.

Kwa Biden kujiondoa katika kampeni ya kuchaguliwa tena, mpango wa Republican ulioongozwa na Donald Trump umegeuzwa kuwa juu chini.

Warepublican walitumia wiki nzima ya matukio yaliyoandikwa kwa makini yakiangazia udhaifu wa mtu wanayetaka kumpinga.

Kampeni hiyo ilikuwa imeangazia nguvu na uchangamfu wa mgombeaji wao kwa kumtanguliza katika ukumbi mwana mieleka wa zamani Hulk Hogan na mpiganaji wa Ultimate Fighting Championship Dana White, pamoja na onyesho la Kid Rock.

.

Chanzo cha picha, Reuters

Maelezo ya picha, Hulk Hogan katika kongamano la Republican

Jaribio la kutofautisha udhaifu wa Bw Biden – na mkakati wa kuwavutia wapiga kura wachanga – lilikuwa dhahiri.

Lakini katika hali yoyote sasa, mteule wa Democrats atakuwa mtu mwenye mdogo zaidi kuliko rais.

Mkakati wa nguvu dhidi ya dhaifu dhidi ya Makamu wa Rais Kamala Harris au mmoja wa magavana wachanga zaidi wa Democrats ambao wanatajwa kuwa warithi wa Biden hawataweza kuwa na nguvu sawa na Biden.

Iwapo Harris ndiye mteule, tarajia Republicans kujaribu kumfungamanisha na makosa yanayoonekana ya utawala uliopo.

Kwa miezi kadhaa wamemwita “mfalme wa mpaka”.

Ingawa mwendesha mashtaka huyo wa zamani hatokani na mrengo unaoendelea wa chama, mashambulizi ya hapo awali ya Republican dhidi yake yanadokeza kwamba yanaweza pia kumtia doa kama mtu anayegemea “mrengo wa kushoto”.

Haijalishi ni nani atakayeteuliwa, Republicans wana uhakika wa kulaumu Democrats kwa kufunika udhaifu wa Biden unaohusiana na umri – na kuweka taifa katika hatari.

Kwa wakati huu, imesalia miezi michache tu hadi kura za kwanza za urais zipigwe.

Imetafsiriwa na Seif Abdalla