Dar es Salaam. Ukiulizwa kitu gani kigumu kwenye muziki kwa miaka hii, majibu watakayokupa ni pamoja na kuzipata collabo kwa wanamuziki wakubwa nchini kama Diamond Platnumz, Ali Kiba, Rayvanny, Nandy na wengineo.
Lakini kwa mwanamuziki Jay mwenye Melody zake imekuwa tofauti siyo tu amefanikiwa kuzipata kolabo bali hajazitafuta yeye wao ndio wamemtafuta kufanya naye kazi.
Jay Melody amefanikiwa kufanya kazi kwa ukaribu na wasanii wakubwa ambao wameteka kiwanda cha Bongo Fleva, tena kwa kushirikishwa, kitu ambacho kinazidi kumpa heshima kwenye muziki wake.
‘Mapozi’ ya kwake Diamond Platnumz akiwa na Mr.Blue hii ni toleo la pili baada ya wimbo orijino wa Mr.Blue uliotoka mwanzoni mwa miaka ya 2000, maoni mengi ya mashabiki kuhusiana na wimbo huo wanaonesha kupendezwa na verse ya Jay Melody ambaye ndiye anaanza kufungua ngoma hiyo.

Mapozi ni miongoni mwa ngoma kali za Bongo Fleva kuwahi kutokea, ukiwa na watazamaji milioni 22 kwenye mtandao wa YouTube, wimbo huo umewakutanisha manguli wa muziki kwa hiyo kwa Jay Melody kuwepo tu kwenye ngoma hiyo ni kitu kikubwa kwenye muziki wake
Dance ya kwake Rayvanny (Chui) akiwa amemshirikisha Jay Melody, mwaka mmoja uliopita Rayvanny alishindwa kukamilisha mradi wake wa EP (Extended Playlist) ya FLOWERS III mpaka alipopata verse ya Jay Melody kwenye track no 3 inayoenda kama Dance kwenye EP hiyo iliyotoka 2023.

Jay Melody anaendelea kuonesha hatari yake kwenye muziki wa Bongo Fleva baada ya kupewa nafasi ya kushiriki kwenye EP ya ‘Starter’ kutoka kwa mkali wa Bongo Fleva Mfalme Ali Kiba. Hatari ni track namba 4 kwenye EP ya Starter ikiwa ni ngoma ya Bongo Fleva yenye Melody kali kutokana na wakali hao kuwa na muunganiko ulio bora.
Ukiachilia mbali JayMelody kushirikishwa na wasanii wa kiume pia hata wasanii wa kike wamemshirikisha kwenye baadhi ya nyimbo zao kama Phina ngoma inayoitwa ‘Manu’ iliyotoka Novemba 27, 2023
Utakumbuka kuwa Jay Melody alipita Tanzania House of Talent (THT), kwa ajili ya kukuza kipaji chake cha muziki, jina lake kwenye sanaa alipewa na Ruge Mutahaba ambaye alikuwa msimamizi wa kituo hicho kilichowatoa mastaa kama Mwasiti, Barnaba, Linah, Amini, Nandy n.k.

Jay Melody hadi sasa ametoa albamu moja, Therapy (2024) na kushinda TMA 2022, alitoka na kibao chake, Goroka (2018).