
MSHAMBULIAJI wa Ain Diab ya Morocco, Jaruph Juma amesema msimu uliopita haukuwa bora kwa upande wake akitaja uchovu na kutofanya mazoezi vilimkwamisha kuanza vizuri.
Ain inashiriki Ligi Kuu ya Soka la Ufukweni nchini Morocco ambapo Mtanzania huyo alijiunga nayo wakati ligi inaenda mwishoni.
Licha ya kutoanza vizuri lakini kwenye michezo 10 aliyocheza Jaruph amefunga mabao manane.
Akizungumza na Mwanaspoti, Jaruph anaamini kama msimu huu ataanza maandalizi mapema basi huenda akaandika historia nchini Morocco. “Michezo miwili ya kwanza nimecheza na uchovu wa safari, lakini nashukuru muda ulivyozidi kwenda nikakaa sawa, sikuwa kwenye kiwango changu bora zaidi kwasababu ya ugeni,” alisema na kuongeza:
“Sikuwahi kufanya mazoezi na timu, pia falsafa za mwalimu kwahiyo kutofahamiana kimifumo ya uchezaji ilikuwa changamoto, magoli mengi niliyofunga yametokana na uwezo binafsi sio muunganiko wa timu.”
Mshambuliaji huyo aliwahi kukipiga soka la kawaida akizitumikia Simba (2016), Yanga U-20 (2015), African Lyon kwa misimu mitatu kuanzia 2019 hadi 2021.