
Mawaziri wa mambo ya nje wa Japani, Korea Kusini na China wamekubaliana siku ya Jumamosi, Machi 22, kuimarisha ushirikiano wao, amesema mkuu wa diplomasia ya Japani, Takeshi Iwaya, huku kukiwa na shinikizo la kibiashara kutoka Marekani.
Imechapishwa:
Dakika 2
Matangazo ya kibiashara
“Hali ya kimataifa imezidi kuwa ngumu, na si kukithirisha kusema kwamba tuko katika hatua ya mabadiliko katika historia,” amesema Waziri wa Mambo ya Nje wa Japani Takeshi Iwaya, akifungua mazungumzo na viongozi wenzake wa China Wang Yi na Korea Kusini Cho Tae-yul. “Ni muhimu zaidi kuliko hapo awali kuzidisha juhudi za kushinda migawanyiko na makabiliano kupitia mazungumzo na ushirikiano.”
“Tumekuwa na mazungumzo kuhusu ushirikiano wa pande tatu na masuala ya kikanda na kimataifa kwa mtazamo mpana, na tumethibitisha kwamba tutakuza ushirikiano wenye mwelekeo wa siku zijazo,” mkuu wa diplomasia ya Japani, Takeshi Iwaya, amewaambia waandishi wa habari baada ya mkutano wa pande tatu huko Tokyo.
“Kupambana pamoja”
Kuimarisha ushirikiano kutatuwezesha “kupinga hatari kwa pamoja” na kukuza “maelewano ya pamoja” kati ya raia, Wang Yi amebainisha. Mkutano huu wa pande tatu, wa 11 katika muundo huu, unakuja wakati Asia ya Mashariki ikijipata chini ya tishio la forodha la Rais wa Marekani Donald Trump, na inakabiliwa na kutumwa kwa wanajeshi wa Korea Kaskazini kuunga mkono Urusi nchini Ukraine na luteka ya Beijing kuzunguka Taiwan.
Wang Yi ametangaza kwamba Tokyo, Seoul na Beijing zinakusudia “kuharakisha” majadiliano yao ili kuandaa mkutano mpya kati ya viongozi wao. Wakuu wa nchi au serikali za nchi hizo tatu walikutana mjini Seoul mnamo mwezi Mei 2024 kwa mkutano wao wa kwanza wa pande tatu katika kipindi cha miaka mitano, ambapo walithibitisha tena lengo lao la kumaliza mpango wa nyuklia katika rasi ya Korea – wakimaanisha silaha za nyuklia zilizotengenezwa na Korea Kaskazini.
Korea Kaskazini
Seoul na Tokyo zinaonyesha msimamo mkali zaidi dhidi ya Pyongyang kuliko Beijing, ambayo inasalia kuwa moja ya washirika wakuu na waungaji mkono wa kiuchumi wa Korea Kaskazini. “Tulisisitiza tena kwamba kudumisha amani na utulivu kwenye rasi ya Korea ni maslahi ya pamoja na wajibu wa pamoja wa nchi hizo tatu,” Cho Tae-yul amesema baada ya mkutano wa Jumamosi. “Hata hivyo, nimesisitiza kwamba ushirikiano haramu wa kijeshi kati ya Urusi na Korea Kaskazini lazima ukomeshwe mara moja,” ameongeza.
Wakati Beijing imesogea karibu zaidi na Moscow tangu ilipoanzisha uvamizi wake kamili dhidi ya Ukraine miaka mitatu iliyopita, waziri wa mambo ya nje wa Japan ameonya kwamba haikubaliki “popote” “kubadilisha hali iliyopo kwa nguvu.” Mawaziri hao pia wamejadili mabadiliko ya Tabianchi na hatua za kukabiliana na kupungua kwa kiwango cha kuzaliwa, pamoja na ushirikiano wa kiteknolojia na usaidizi kwa wahasiriwa wa majanga ya asili.