Japan, Tanzania zaikumbuka sekta ya mpunga

Dodoma. Wakati uzalishaji wa zao la mpunga ukiongezeka kwa asilimia tano kutoka mwaka 2010, wadau nchini wametakiwa kuzichangamkia fursa zinazopatikana kwenye mnyororo mzima wa thamani wa zao hilo ambalo ni la pili kwa kukua kwa kasi.

Hayo yamebainishwa na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo anayesimamia Maendeleo ya Mazao na Usalama wa Chakula, Dk Hussein Omar wakati akifunga mkutano wa kitaifa wa wadau wa zao la mpunga kwa niaba ya Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Gerald Mweli.

Mkutano wa Mwaka wa mapitio ya Sekta ya Mpunga (ARSRM), umefanyika hivi karibuni jijini Dodoma na kuwakutanisha Shirika la Kimataifa la Ushirikiano la Japan (JICA) na Serikali ya Tanzania na wadau.

Kulingana na Mkakati wa Kitaifa wa Maendeleo ya Zao la Mpunga wa Tanzania Awamu ya Pili (NRDS-2: 2019-2030), mkutano huo umetathmini maendeleo, kubaini mapungufu ya rasilimali, na kupanga mikakati ya kuifanya Tanzania kuwa kiongozi wa soko la mchele katika kanda.

Dk Omar amesema tija ya zao hilo inatarajiwa kuongezeka kutoka tani mbili kwa hekta hadi kufikia tani 4.4 kwa hekta katika kilimo cha mvua na tani 7.34 kwa hekta katika kilimo cha umwagiliaji.

Amebainisha kuwa zao la mpunga ni zao la pili linalokua kwa kasi nchini huku uzalishaji wake ukiongezeka kwa asilimia tano kutoka mwaka 2010 huku  asisitiza tija ya zao hilo inatarajiwa kuongezeka kutoka tani 2 kwa hekta kufikia tani 4.4 kwa hekta, katika kilimo cha mvua na tani 7.34 kwa hekta katika kilimo cha umwagiliaji.

Dk Omar, amesisitiza Serikali imefanya juhudi ikiwa ni pamoja na kuboresha miradi 55 ya umwagiliaji, kujenga mabwawa 14, kupanua maghala ili kupunguza hasara baada ya mavuno, na kuboresha upatikanaji wa mbegu zinazostahimili mabadiliko ya tabianchi na kuanzisha mifumo ya usajili wa wakulima.

Naye Katibu Tawala Msaidizi – Uchumi na Uzalishaji katika Mkoa wa Tabora, Abrahaman Mndeme amesema lengo la Serikali ni kuongeza uzalishaji wa zao la mpunga kutoka tani milioni nne za sasa na kufikia tani milioni saba ifikapo 2030.

Kwa upande wake, Ara Hitoshi, Mwakilishi Mkuu wa JICA Tanzania, amesisitiza umuhimu wa Serikali katika kushika jukumu la kuratibu wadau:

“Ushirikiano huu ni muhimu ili kukabiliana na changamoto mbalimbali, kukusanya nguvu na kuendeleza utoshelevu wa zao la mpunga kwa Tanzania wakati nchi ikiendeleza kuongoza katika kanda,” amesema.

Amesema ushindani kwenye uzalishaji wa zao la mpunga unaongezeka na utasaidia kufanikisha azima ya Serikali ya kukuza zaidi kilimo cha zao hilo.

ARSRM imejumuisha mijadala kuhusu maendeleo ya NRD5-II, mwenendo soko, na fursa za uwekezaji, kutoa jukwaa la kushirikishana mafanikio na changamoto katika minyororo ya thamani.

Aidha, JICA imethibitisha azima yake kupitia (CARD), kuwa kusaidia Tanzania na nchi nyingine 31 za Afrika katika utekelezaji wa mikakati ya kuongeza ustahimilivu wa mabadiliko ya tabianchi, na uwezeshaji wa mnyororo ya thamani wa zao hilo.

Mkutano huo umesisitiza hatua za Tanzania katika kuhakikisha ina usalama wa chakula, ajira na ukuaji wa kiuchumi kupitia maendeleo ya sekta ya mchele, huku wadau wakiahidi kushirikiana zaidi ili kufikia malengo ya NRDS-IL

Katika hatua nyingine Dk Omar ameishukuru Serikali kwa kupandisha bajeti ya Wizara ya Kilimo kutoka Sh294 bilioni kwa mwaka wa fedha 2021/2022 hadi kufikia Sh1.2 trilioni kwa mwaka wa fedha 2024/2025, ambapo ongezeko hilo la bajeti ya izara inachangia kuongezeka kwa tija katika uzalishaji wa zao la mpunga.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *