
Dar es Salaam. Mgombea wa Tanzania kwa nafasi ya Mkurugenzi wa Kanda wa Shirika la Afya Duniani (WHO) kwa Afrika, Profesa Mohammed Janabi, amewasilisha maono yake kwa nafasi hiyo, akisisitiza dhamira yake ya kuhakikisha utekelezaji wa Azimio la Abuja.
Azimio hilo la mwaka 2001 linazitaka nchi wanachama wa WHO barani Afrika kutenga angalau asilimia 15 ya bajeti zao kwa sekta ya afya. Profesa Janabi ameahidi kushawishi mataifa yote wanachama kuhakikisha wanatekeleza azimio hilo kikamilifu.
Akizungumza leo Jumatano, Aprili 2, 2025, wakati wa kunadi sera zake mbele ya wajumbe wa mkutano mkuu wa WHO wanaojiandaa kupiga kura Mei 18, Profesa Janabi ameeleza mipango yake ya kuzishawishi serikali za Afrika kuongeza bajeti ya afya kwa ajili ya dawa na huduma za msingi.
Katika mdahalo wa moja kwa moja wa wagombea wa nafasi hiyo, Profesa Janabi, ambaye anachuana na wagombea wengine wanne, ameeleza kwa nini anafaa kushika wadhifa huo, huku akitaja vipaumbele saba atakavyoshughulikia endapo atachaguliwa.
Akitaja uzoefu wake, amesema akiwa Mkurugenzi Mtendaji wa kwanza wa Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) mwaka 2024, alifanikiwa kupunguza kwa asilimia 95 idadi ya wagonjwa waliokuwa wakipelekwa nje ya nchi kwa matibabu, hatua iliyoipunguzia Tanzania gharama ya zaidi ya Dola milioni 10 kwa mwaka.
Fedha hizo ziliwekezwa katika kuimarisha huduma za Afya ya Msingi (PHC), zikilenga kusaidia wananchi wasio na uwezo wa kugharamia matibabu hospitalini.
Amesema mafanikio hayo yalitokana na uboreshaji wa uwezo wa ndani wa wataalamu, kuimarisha miundombinu, kuongeza bajeti ya afya, kushirikiana na sekta binafsi, na kukuza ushirikiano wa kimataifa.
“Leo hii, JKCI ni kituo cha kikanda kinachofanya zaidi ya upasuaji wa moyo wazi na matibabu ya moyo kwa wagonjwa 4,000 kila mwaka, wakiwemo wanaopatiwa huduma za upandikizaji wa betri za moyo (pacemakers) na upasuaji mwingine wa hali ya juu, wakiwemo wagonjwa kutoka mataifa mbalimbali ya Afrika,” amesema.
Profesa huyo amesema mwaka 2022, aliteuliwa kuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), mojawapo ya hospitali kubwa zaidi katika kanda hiyo, ikiwa na vitanda zaidi ya 2,400 na wafanyakazi zaidi ya 4,000, na kuhudumia wastani wa wagonjwa 3,000 kwa siku.
“Mbali na hayo, ninasimamia mtandao wa vituo vidogo vya afya 12,200 nchini kupitia tiba mtandao, tiba-elektroniki, na matumizi ya akili bandia. Malengo yetu ni kuwafundisha wahudumu wa afya wa jamii 137,000 ifikapo mwaka 2030 ili kuwa kiungo kati ya jamii na mfumo rasmi wa afya,” amesema.
Chini ya uongozi wake, Profesa Janabi amesema, Muhimbili ilipata ufadhili wa Dola milioni 363 za Marekani (sawa na Sh962.8 bilioni) mwaka 2025 kutoka Jamhuri ya Korea Kusini kwa masharti ya nafuu—riba ya asilimia 0.01, kipindi cha neema cha miaka 15, na muda wa kulipa wa miaka 25 kwa ajili ya kuimarisha mfumo wa afya.
“Ufadhili huu wa kibunifu utaifanya Muhimbili na vituo vyake vya afya kuwa kitovu cha kikanda cha huduma za kinga, tiba, ulinzi na urejeshaji wa afya,” amesema.
Endapo atachaguliwa kuwa Mkurugenzi wa WHO Kanda ya Afrika, ameahidi kushirikiana na wafadhili wa aina hiyo kutoka Afrika na kwingineko ili kuimarisha huduma za afya barani.
Vipaumbele Saba
Profesa Janabi ameeleza vipaumbele vyake saba, akianza na upatikanaji wa huduma za afya kwa wote (UHC) unaoendana na Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs), akibainisha kuwa Afrika imechelewa katika utekelezaji wake.
Kipaumbele cha pili ni ufadhili endelevu, ambapo ameeleza kuwa nchi wanachama huchangia asilimia 20 pekee ya bajeti ya WHO.
Hali hiyo, amesema, inazuia uhuru wa shirika hilo, hivyo anaunga mkono kuongeza michango ya lazima na kupanua vyanzo vya fedha kupitia bima ya afya, ubia kati ya sekta ya umma na binafsi, uwekezaji mseto, ubadilishaji wa madeni kwa afya, na kufutwa kwa madeni ya kimataifa.
Kipaumbele cha tatu ni maandalizi ya kukabiliana na dharura za kiafya, ambacho kinajumuisha kuimarisha nguvu kazi ya afya, kuboresha ufuatiliaji wa magonjwa, kuimarisha mifumo ya mwitikio wa haraka, na kukuza ushirikiano wa mipakani.
Katika afya ya mama, mtoto na lishe, amesema Afrika inachangia asilimia 70 ya vifo vya wajawazito na asilimia 56 ya vifo vya watoto chini ya miaka mitano duniani.
Hata hivyo, Tanzania ilipunguza vifo vya wajawazito kwa asilimia 80 kati ya 2015 na 2022, mafanikio yaliyotambuliwa wakati Rais Samia Suluhu Hassan alipokea Tuzo ya Global Goalkeeper kutoka Taasisi ya Gates mwaka 2024.
Profesa Janabi pia ameahidi kupambana na magonjwa ya kuambukiza, yasiyoambukiza na magonjwa yaliyopuuzwa kwa kutekeleza mikakati thabiti ya kudhibiti magonjwa, kukuza maisha yenye afya, na kutambua uhusiano kati ya binadamu, wanyama, mimea na mazingira.
Kipaumbele cha sita ni kupambana na usugu wa vimelea vya dawa (AMR), tatizo linalosababisha vifo milioni 1.2 kila mwaka, huku asilimia 40 ya mataifa ya Afrika yakikosa takwimu za ufuatiliaji. Ameahidi kuanzisha hifadhidata za kikanda kukabiliana na tatizo hilo.
Kipaumbele cha saba ni kuimarisha uwezo wa uzalishaji wa ndani wa bidhaa za afya. Amesema janga la Uviko-19 lilidhihirisha utegemezi mkubwa wa Afrika kwa uagizaji wa dawa, chanjo na vifaa tiba, ambapo zaidi ya asilimia 99 ya bidhaa hizo zilikuwa zinatoka nje.
“Nitatumia diplomasia ya afya kuimarisha ushirikiano wa mifumo ya afya na kuinua uongozi wa Afrika katika afya ya kimataifa,” amesema.
Utafiti na utetezi
Profesa Janabi amesema miaka ya 2000, alishiriki katika tafiti za majaribio ya VVU kati ya Tanzania na Msumbiji.
Kazi yake mwaka 2012 ilisababisha Rais wa wakati huo, Jakaya Kikwete, kufanyiwa vipimo vya VVU hadharani, hatua iliyosaidia kuondoa unyanyapaa na kuwahamasisha Watanzania milioni tano kupima na kupata ushauri nasaha.
Hali kama hiyo ilijitokeza tena mwaka 2021, Rais Samia Suluhu Hassan alipojitokeza hadharani kuhimiza chanjo ya Uviko-19, hatua iliyoongeza kwa kiasi kikubwa uchanjaji na kupunguza upotoshaji wa taarifa.
Profesa Janabi pia alikumbuka tukio la mwaka 2015 kutokana na mlipuko wa ugonjwa wa Ebola Afrika Magharibi. Wakati huo, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-moon, alimteua Rais Kikwete kuongoza Jopo la Ngazi ya Juu la Umoja wa Mataifa kuhusu Migogoro ya Afya Duniani.
Akiwa mshauri mwandamizi, Profesa Janabi alitembelea maeneo yaliyoathirika huko Liberia, Guinea, na Sierra Leone, akipata uzoefu wa moja kwa moja wa kukabiliana na janga hilo.
“Mapendekezo ya jopo hilo yalisababisha mabadiliko ya mbinu ya WHO katika kushughulikia dharura za afya,” amesema Profesa Janabi.
Amesisitiza kuwa idadi kubwa ya vijana barani Afrika inatoa fursa na changamoto. “Ingawa vijana wanachochea ukuaji na uvumbuzi, wanakabiliwa na hatari kama vile matumizi ya dawa za kulevya, ngono isiyo salama, mimba za utotoni, na matatizo ya afya ya akili,” amesema.
Wakati huohuo, ameeleza umuhimu wa kuandaa mifumo ya afya kwa ajili ya idadi inayoongezeka ya wazee.
WHO Afrika ina jumla ya nchi wanachama 47 ambao wanatarajiwa kupiga kura kumchagua mkurugenzi wa shirika hilo barani Afrika kuziba nafasi ya mshindi wa nafasi hiyo, Mtanzania, Dk Faustine Ndugulile, aliyefariki dunia kabla ya kuanza kutekeleza majukumu yake.