Dar es Salaam. Wakati magonjwa yasiyoambukiza ikiwamo saratani yakitajwa kushamiri nchini, jamii imeaswa kuwakumbuka wanawake wenye ugonjwa huo kwa mahitaji na kuwapa moyo.
Kwa mujibu wa takwimu ya Shirika la Afya Duniani (WHO), hadi mwaka 2022, kulikuweko na wagonjwa wapya milioni 20 wa saratani na kati yao hao milioni 9.7 walifariki dunia.
Hayo yamesemwa na Meneja Mkuu wa SICPA Tanzania, Alfred Mapunda pamoja na wafanyakazi wanawake wa taasisi hiyo walipoenda kutoa msaada kwa wagonjwa wa saratani katika Taasisi ya Saratani ya Ocean Road jijini Dar es Salaam.
SICPA wametoa msaada huo Machi 7, 2025 katika kuadhimisha siku ya wanawake duniani.
“Kwenye SICPA Tanzania, tunaamini katika kutumia rasilimali zetu siyo tu kwa kuendeleza ubunifu na usalama wa uzingatiaji wa kodi, bali pia kuinua jamii na kuboresha maisha ya watu.
“Katika Siku hii ya Wanawake, tunatambua nguvu na ustahimilivu wa wanawake wanaopambana na saratani, na tunajivunia kuwaunga mkono kupitia msaada huu,” amesema na kuongeza Mapunda

Wafanyakazi wa SICPA Tanzania wakiwa katika Hospitali ya Ocean Road
Mapunda amesema msaada huo umelenga kupunguza changamoto wanazokumbana nazo wagonjwa wa saratani pamoja na familia zao.
Ameongeza kuwa: “Dhamira ya kampuni katika kuhudumia umma inakwenda zaidi ya uzingatiaji wa kodi, kama inavyoonyeshwa kupitia juhudi kama hii ya msaada wa Siku ya Wanawake.”