Kwa miaka mingi, Jamhuri Park maarufu kama Forodhani ilikuwa sehemu isiyopewa kipaumbele jijini Tanga, ikiachwa na nyasi kavu, taka, na ukosefu wa usimamizi madhubuti. Lakini leo hii, bustani hiyo ya ekari 7.7 iliyoko barabara ya Uhuru mjini Tanga, ni mfano hai wa mabadiliko yanayowezekana kupitia ushirikiano wa jamii na uongozi wenye maono.
“Kuhusu Jamhuri Park, tulikuwa tunaona ni sehemu ya kupita tu, hakukuwa na chochote cha kutuvutia,” anasema Zuhura Hassan, mkazi wa Mwanzange. “Sasa, kila Jumamosi tunakuja hapa kupumzika na watoto.” Ushuhuda wa Zuhura unaakisi maelfu ya wakazi wa Tanga waliopokea kwa mikono miwili ukarabati wa bustani hiyo chini ya programu ya TangaYetu.
Kabla ya mwaka 2023, Jamhuri Park haikuwa kivutio tena. Iliathirika na uchakavu, kutotunzwa, na ukosefu wa huduma muhimu kama taa, vyoo vya kisasa, na maeneo ya michezo kwa watoto. Bustani hiyo haikuchangia chochote kwenye pato la Halmashauri ya Jiji la Tanga.

Muonekano wa kauvutia katika eneo la Jamhuri Park maarufu kama Forodhani.
Kupitia programu ya TangaYetu, kwa ushirikiano na Halmashauri ya Jiji la Tanga, bustani hiyo ilifanyiwa mchakato jumuishi uliohusisha wananchi, vijana, na wadau wengine kupanga kwa pamoja muundo mpya wa bustani hiyo. Mradi huo ulijumuisha upembuzi yakinifu, uandaaji wa mpango wa biashara, na ukarabati mkubwa wa miundombinu.
“Lengo letu halikuwa tu kuboresha miundombinu ya mijini,” anasema Prof. Ally Namangaya, aliyesimamia awamu ya usanifu wa bustani hiyo. “Tulitaka kuleta mabadiliko ya kweli kuhusu jinsi miji yetu inavyowahudumia wakazi wake, hasa vijana. Leo hii, Jamhuri Park si bustani tu, bali pia ni kitovu cha biashara, burudani kwa watoto na vijana, na umoja wa jamii”.
Bustani kwa sasa ina sehemu za kijani za kupumzika, maeneo ya michezo ya watoto yenye vifaa vya kisasa, vibanda vya biashara kwa wajasiriamali vijana, taa zinazotumia nishati ya jua, na mfumo wa usimamizi wa taka. Watoto hushiriki michezo, watu wazima hukutana kwa mazungumzo na kupunga upepo wa Bahari ya Hindi, na wafanyabiashara huuza bidhaa mbalimbali.
Kwa mujibu wa Bwana Jonas Ngwatu, Afisa Biashara wa Jiji la Tanga na msimamizi wa bustani hiyo, zaidi ya vijana 50 wamepata nafasi za kuendesha biashara zao ndani ya bustani hiyo. “Jamhuri Park ni sehemu ya kukaribisha watu wa rika zote. Watoto wanafurahia michezo, wazazi wanapumzika, na vijana wanauza bidhaa zao kwenye vibanda rasmi,” anasema.
Wakati wa ujenzi, zaidi ya vijana 30 walihusishwa kwenye kazi za muda mfupi katika ujenzi, usafi hadi kazi za kiufundi. Bustani hiyo pia imekuwa sehemu kuu ya matukio ya kijamii, mikutano na tamasha, jambo lililoongeza mapato ya Halmashauri ya Jiji la Tanga kwa kiasi kikubwa.
Meya wa Tanga, Mhe. Abdurahman Shiloow, anasema, “Jamhuri Park inaakisi dhamira ya Tanga ya kuleta maendeleo na mshikamano. Hili ni darasa kwa miji mingine nchini.”
Jamhuri Park imekuwa somo la jinsi maeneo ya umma yakitumiwa vizuri yanaweza kuimarisha mshikamano wa jamii, kukuza uchumi wa ndani, na kuwapa vijana nafasi ya kujitegemea. Mradi huu umekuwa mfano kwa miji kama Dodoma, Tunduma, na Mwanza ambapo maeneo ya wafanyabiashara wadogo yameanzishwa kwa kuiga mfumo huu wa ushirikishwaji.
Kwa Tanga, bustani hii sasa ni ahadi iliyotimizwa. Inawakumbusha wananchi kwamba mabadiliko yanawezekana pale ambapo jamii na viongozi wanashirikiana.
Programu ya TangaYetu inafadhiliwa na Fondation Botnar na inatekelezwa na kampuni ya INNOVEX (www.innovexdc.com) kwa kushirikiana na Halmashauri ya Jiji la Tanga, ikiifanya Tanga kuwa jiji ambalo vijana wanastawi.