Jamaa wameupiga mwingi Ligi Kuu Bara

WAKATI Ligi Kuu Bara inatarajiwa kurejea Jumanne, Aprili Mosi baada ya kupisha kalenda ya mechi za kimataifa kwa timu za taifa. Siku hiyo utapigwa mchezo mmoja na mabingwa watetezi Yanga itakuwa mgeni wa Tabora United kwenye Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi, Tabora.

Katika ligi hiyo ambayo imefika raundi ya 23 hadi sasa huku Yanga na Simba zikicheza 22, wapo wachezaji, makocha na mameneja waliofanya vizuri katika raundi hizo katika mechi na kubeba tuzo na hapa Mwanaspoti linakuletea makala ya waliong’ara hadi sasa tangu Ligi Kuu Bara ilipoanza Agosti mwaka jana.

AGOSTI 2024

Kiungo wa Simba, Jean Charles Ahoua alishinda tuzo ya mchezaji bora wa Ligi Kuu Bara Agosti, baada ya timu hiyo kupata ushindi katika michezo miwili iliyocheza, huku akichangia mabao manne akifunga moja na kuasisti mengine matatu.

Kwa mwezi huo, Simba ilianza ligi kwa ushindi wa mabao 3-0, dhidi ya Tabora United kisha kuifunga Fountain Gate mabao 4-0.

Kwa upande wa tuzo ya kocha bora ilienda kwa Fadlu Davids wa Simba aliyewashinda Patrick Aussems aliyekuwa Singida Black Stars na Abdallah Mohamed ‘Baresi’ wa Mashujaa FC aliyetimuliwa rasmi Februari 26, mwaka huu kutokana na mwenendo mbaya.

Tuzo ya meneja bora wa uwanja ilienda kwa Ashraf Omar anayehudumia Uwanja wa Meja Isamuhyo unaotumiwa na JKT Tanzania kutokana na kufanya vizuri katika menejimenti ya matukio ya michezo na masuala yote yanayohusu miundombinu ya uwanjani.

SEPTEMBA 2024

Aliyekuwa mshambuliaji wa Fountain Gate, Seleman Mwalimu anayeichezea kwa sasa Wydad Casabalanca ya Morocco, alishinda tuzo hiyo akiwashinda Edgar William aliyecheza naye na Feisal Salum ‘Fei Toto’ wa Azam alioingia nao fainali.

Mwalimu aliisaidia Fountain kushinda michezo mitatu na kutoka sare mmoja, huku akifunga mabao matatu dakika 353 alizocheza.

Tuzo ya kocha bora ilienda kwa Mohamed Muya aliyekuwa Fountain Gate aliyeiongoza kushinda michezo mitatu na kutoka sare mmoja tu, akianza na 2-1, dhidi ya KenGold, (3-1) v Tabora United, (3-1) v Kagera Sugar na sare ya 2-2 na Dodoma Jiji.

Muya aliwashinda Denis Kitambi aliyekuwa Singida Black Stars na Rachid Taoussi wa Azam FC alioingia nao katika fainali hiyo.

Tuzo ya meneja bora wa Septemba ilienda kwa Godwin Israel anayehudumia Uwanja wa Tanzanite Kwaraa unaotumiwa na Fountain Gate.

OKTOBA 2024

Nyota wa Singida Black Stars, Marouf Tchakei alichaguliwa mchezaji bora wa mwezi Oktoba baada ya kukisaidia kikosi hicho kushinda michezo mitatu kati ya minne, huku akifunga mabao matatu na kuasisti moja katika dakika 360 alizocheza.

Michezo iliyoshinda ni (1-0) dhidi ya Mashujaa FC, (2-0) v Namungo FC, (2-0) v Fountain Gate na kupoteza 1-0, mbele ya Yanga.

Tchakei raia wa Togo aliwashinda Lusajo Mwaikenda wa Azam FC na Pacome Zouzoua wa Yanga waliokuwa wanachuana kwa mwezi huo.

Kwa upande wa tuzo ya kocha bora, ilienda kwa Rachid Taoussi wa Azam FC baada ya kukiongoza kikosi hicho kushinda michezo yote mitatu aliyoiongoza akianza na (1-0) v Namungo FC, (2-0) v Tanzania Prisons na kuichapa pia KenGold kwa mabao 4-1.

Katika tuzo hiyo, Taoussi aliwashinda washindani wake, Abdihamid Moallin aliyekuwa anaifundisha KMC FC kwa wakati huo kabla ya kujiunga na mabingwa watetezi wa Ligi Kuu Yanga na Denis Kitambi aliyekuwa anaifundisha Singida Black Stars.

Pia, kamati ya tuzo ilimchagua Godwin Israel kuwa meneja bora wa Uwanja wa Tanzanite Kwaraa uliopo Babati unaotumiwa na Fountain Gate.

NOVEMBA 2024

Mshambuliaji wa Tabora United, Offen Chikola alichaguliwa mchezaji bora wa Novemba baada ya kuisaidia timu hiyo kushinda michezo mitatu kati ya minne iliyocheza huku akifunga mabao matatu kwa mwezi huo katika dakika 351 alizocheza kikosini.

Tabora ilizifunga Yanga mabao 1-3, Mashujaa (1-0), KMC (0-2) na ikatoka sare ya 2-2 na Singida Black Stars na kukusanya pointi 10, huku akiwashinda nyota mwenzake, Yacouba Songne na Moussa Camara wa Simba alioingia nao katika fainali hiyo.

Kwa upande wa tuzo ya kocha bora ilienda kwa Rachid Taoussi wa Azam FC baada ya kukiongoza kikosi hicho kushinda michezo yote mitatu, ambapo timu hiyo ilizifunga Singida Black Stars mabao 2-1, kisha kuzichapa bao 1-0, Yanga na Kagera Sugar.

Katika tuzo hiyo, Taoussi aliwashinda washindani wake, Fadlu Davids anayeifundisha Simba na Ahmad Ally wa Maafande wa JKT Tanzania.

Pia, kamati ya tuzo ilimchagua Shaaban Rajabu kuwa meneja bora wa Uwanja wa Lake Tanganyika mkoani Kigoma unaotumiwa na Mashujaa FC.

DESEMBA 2024

Mshambuliaji wa Yanga, Clement Mzize alichaguliwa mchezaji bora wa Desemba baada ya kuisaidia timu hiyo kushinda michezo minne iliyocheza, huku akifunga mabao manne na kuasisti mengine matatu kwa mwezi huo, baada ya kucheza dakika zake 288.

Kwa mwezi huo, Yanga ilizifunga Tanzania Prisons mabao 4-0, (4-0) v Dodoma Jiji, (3-2) v Mashujaa FC na (5-0) v Fountain Gate, huku Mzize akimshinda nyota wenzake, Prince Dube na Feisal Salum ‘Fei Toto’ wa Azam FC ambao aliingia nao fainali.

Kwa upande wa tuzo ya kocha bora ilienda kwa Saed Ramovic aliyekuwa Yanga baada ya kuiongoza timu hiyo kushinda michezo yote minne na kuitoa nafasi ya tatu hadi ya pili, huku akiwashinda Rachid Taoussi wa Azam FC na Fadlu Davids wa Simba.

Tuzo ya meneja bora wa uwanja ilienda kwa Ashraf Omar anayehudumia Uwanja wa Meja Isamuhyo unaotumiwa na JKT Tanzania, kutokana na kufanya vizuri katika menejimenti ya matukio ya michezo na masuala yote yanayohusu miundombinu ya uwanjani.

FEBRUARI 2025

Januari hakukuwa na ugawaji wa tuzo kutokana na michuano ya Kombe la Mapinduzi ila Februari Ligi Kuu Bara iliporejea tu, nyota wa Yanga, Prince Dube alichaguliwa mchezaji bora, baada ya timu hiyo kushinda michezo sita na kutoka sare mmoja.

Nyota huyo mwenye mabao 10 kwa sasa ya Ligi Kuu Bara, Februari alichangia 10 ya kikosi hicho baada ya kufunga matano na kuasisti pia matano katika dakika 562 alizocheza, akiwa na wastani mzuri wa kufunga na kusaidia upatikanaji wa mengine.

Kwa mwezi huo, Yanga ilizifunga KMC FC mabao 6-1, (2-1) v Singida Black Stars, (5-0) v Mashujaa FC, (3-0) v Pamba FC, (6-1) v KenGold, (4-0) v Kagera Sugar, huku mchezo pekee wa suluhu (0-0), ulikuwa ni dhidi ya Maafande wa JKT Tanzania.

Katika tuzo hizo, Dube alimshinda nyota mwenzake, Stephane Aziz KI na Selemani Bwenzi wa KenGold alioingia nao kwenye fainali.

Kwa upande wa tuzo ya kocha bora ilienda kwa Miloud Hamdi wa Yanga baada ya kuiongoza timu hiyo kushinda michezo minne na kutoka sare mmoja kati ya saba iliyocheza na kuwashinda Fadlu Davids wa Simba na Fredy Felix ‘Minziro’ wa Pamba FC.

Tuzo ya meneja bora wa uwanja ilienda kwa Ashraf Omar anayehudumia Uwanja wa Meja Isamuhyo unaotumiwa na JKT Tanzania, kutokana na kufanya vizuri katika menejimenti ya matukio ya michezo na masuala yote yanayohusu miundombinu ya uwanjani.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *