Jaji Warioba, Mongella wataja mageuzi aliyofanya Mzee Msuya

Dar es Salaam. Makamu wa Kwanza wa Rais na Waziri Mkuu mstaafu, Cleopa Msuya, amefariki dunia, huku viongozi waliowahi kufanya naye kazi wakimtaja kuwa mwamba aliyefanikisha kurejea kwa Serikali za Mitaa.

Msuya amefariki dunia jana, saa 3 asubuhi katika Hospitali ya Mzena jijini Dar es Salaam, alikokuwa akipatiwa matibabu ya maradhi ya moyo aliyougua kwa muda mrefu.

Akitangaza taarifa ya msiba huo jana, Rais Samia Suluhu Hassan amesema Msuya amesumbuliwa na tatizo la moyo kwa kipindi kirefu na kupata matibabu ndani ya nchi katika Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete, Mzena na London nchini Uingereza.

“Natoa pole kwa familia, ndugu, jamaa na marafiki kwa msiba huu mkubwa kwa Taifa, na natangaza siku saba za maombolezo kuanzia tarehe 7 hadi 13 (Mei), bendera zitapepea nusu mlingoti,” amesema Rais Samia.

Amesema taarifa zaidi kuhusu msiba huo zitaendelea kutolewa na Serikali.

Msuya amefikwa na umauti akiwa na miaka 94. Alizaliwa Januari 4, 1931 katika Kijiji cha Chomvu Usangi, Wilaya ya Mwanga, Mkoa wa Kilimanjaro.

Msuya alionekana hadharani Machi 9 na 10, 2025 katika matukio tofauti wilayani Mwanga. Machi 9, alihudhuria hafla ya uzinduzi wa mradi mkubwa wa maji wa wilaya tatu za Same- Mwanga- Korogwe uliofanywa na Rais Samia.

Msuya ambaye ni mkazi wa Mwanga, alikuwa amekaa kwenye kiti mwendo na ilielezwa alikuwa miongoni mwa wana Mwanga na Kilimanjaro waliokuwa wakiupigania mradi huo ili ukamilike.

Historia inaonyesha mradi huo wa maji ulitolewa ahadi na Rais wa Awamu ya Nne, Jakaya Kikwete Mei 29, 2005 wakati akiomba kura kuingia madarakani kwa kipindi cha kwanza.

Mradi huo chanzo chake ni Bwawa la Nyumba ya Mungu, ulianza kutekelezwa mwaka 2014 na sasa awamu ya kwanza imekamilika ukiwa umegharimu zaidi ya Sh300 bilioni.

Pia siku iliyofuata, Machi 10, 2025 Msuya alishiriki kwenye mkutano maalumu wa uchaguzi wa Askofu wa Dayosisi ya Mwanga, ya kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT)Dk Daniel Mono, mkutano ambao ulifanyika katika kanisa kuu Mwanga

Mwamba wa kurejea kwa Serikali za mitaa

Akimzungumzia kiongozi huyo, mwanasiasa mkongwe, Balozi Gertrude Mongella, pamoja na kushtushwa na msiba huo, amesema atamkumbuka Msuya kama mwamba aliyefanikisha kurejea kwa Serikali za mitaa.

Wakati Msuya akiwa Waziri Mkuu, Balozi Mongella amesema alikuwa msaidizi wake katika nafasi ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, na ndiye aliyewasilisha muswada bungeni wa kurejeshwa kwa Serikali za mitaa.

“Katika kazi kubwa tuliyofanya naye ni wakati ambao Serikali ilirudisha Serikali za mitaa, ambazo kabla zilikuwa zimesitishwa kwa miaka mingi.

“Kipindi hicho nikiwa waziri katika ofisi yake, nilipeleka muswada uliohusiana na namna ya kupata mapato ndani ya Serikali za mitaa, kwa hiyo nilisimamia urudishaji wa mapato yanayohusu Serikali za mitaa,” amesema.

Amesema haikuwa kazi nyepesi na alifanya hivyo chini ya usimamizi wa Msuya aliyekuwa Waziri Mkuu, hadi kufikia mafanikio yanayoshuhudiwa sasa.

“Kama mnaona Serikali za mitaa sasa, ujue tulifanya wakati wa Msuya, kwa hiyo namkumbuka kama mmoja wa viongozi waliofanikisha kurejea kwa Serikali za mitaa, nami nikiwa msaidizi wake wa karibu, pamoja na wenzangu, Paul Kimiti na Anna Makinda,” ameeleza.

Sambamba na hilo, Balozi Mongella amesema anamkumbuka Msuya kwa juhudi zake za kusaidia masuala ya wanawake, kupitia mkewe Rhoda Msuya.

Warioba amzungumzia

Waziri Mkuu mstaafu, Jaji Joseph Warioba amesema akiwa Chuo Kikuu, Msuya alishakuwa kiongozi ndani ya Serikali kwa nafasi ya Katibu Mkuu.

“…Baadaye nikaingia serikalini na kufanya naye kazi pamoja kwa muda mrefu,” amesema.

Amesema Msuya alikuwa katibu mkuu katika Wizara mbalimbali na baadaye akawa Waziri Mkuu.

“Alipokuwa Waziri Mkuu, mimi nilikuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali na baada ya Mwalimu Nyerere kustaafu, Rais Mwinyi alipoingia akamteuwa kuwa Waziri wa Fedha,” amesema.

Amesema Msuya aliingia kwenye wizara hiyo katika kipindi ambacho, Tanzania ilikuwa ikikabiliwa na hali ngumu ya kiuchumi na ililazimika kufanyika mabadiliko ya kisera.

“Kati ya wasaidizi wa Mwinyi waliokuwa na kazi ngumu alikuwa Waziri wa Fedha na aliyekuwa na nafasi hiyo alikuwa Mzee Msuya,” amesema.

Katika uongozi wa Msuya ndani ya wizara hiyo, Warioba amesema ndipo ilipoanzishwa sera ya soko huria.

Ameeleza kuwa kipindi hicho kulikuwa na lawama za watu wengi ambao hawakupenda sera ibadilishwe na mashirika duniani yaliibana nchi kiasi cha kushindwa kukopa.

“Taasisi zilitubana na haikuwezekana Serikali kukopa popote mpaka majadiliano yafanyike,” amesema.

Amesema Msuya alifanya majadiliano hayo na hatimaye ulifika wakati uchumi uliimarika.

“Ukiona utumishi wa Msuya ameanza kuwa Katibu Mkuu mwaka 1964 hadi mwaka 1995 alikuwa katika uongozi wa nchi na kazi alizofanya zote ni nzuri.

“Mimi nilifanya naye kazi nilikuwa namuamini, pamoja na wakati mwingine mwelekeo ulikuwa tofauti lakini tulimwamini sana Mzee Msuya,” amesema.

Kauli ya RC Kilimanjaro

Akizungumzia kifo cha hayati Msuya, Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Nurdin Babu amesema ni pigo kwa mkoa huo kwa kuwa alikuwa ni msaada na mshauri mkubwa wa masuala ya maendeleo ya mkoa huo.

Amesema hayati Msuya akiwa mapumzikoni mkoani hapa, amekuwa akikaa pamoja naye na kujadili masuala ya maendeleo ya mko.

“Kifo chake tumekipokea kwa mshituko mkubwa na tunampa pole mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan kwa sababu ni kati ya viongozi wakuu wa nchi yetu. Alikuwa Makamu wa Rais na Waziri Mkuu Mstaafu,” amesema RC Babu

Amesema,”Sisi kama wana Kilimanjaro tumepata msiba mkubwa kwa kuondokewa na mzee wetu, Msuya alikuwa msaada mkubwa katika mkoa wetu, mpenda maendeleo na anapokuja huku mapumziko lazima akutane na mimi kuzungumza hali yetu ya mkoa ilivyo.”

Aidha, mkuu huyo wa mkoa ametoa pole kwa wananchi wa Kilimanjaro na Wilaya ya Mwanga kwa kuondokewa na kiongozi huyo nguli nchini.

CCM, Chadema wamlilia

Chama cha Mapinduzi (CCM) na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), vimetoa salamu za pole kutokana na msiba wa Msuya.

Taarifa iliyotolewa jana kwa umma na Katibu Mkuu wa CCM, Dk Emmanuel Nchimbi amesema chama chao kimepokea kwa huzuni taarifa za kifo chake.

“Mzee Msuya alikuwa miongoni mwa makada na viongozi waliotumikia chama, taifa letu na nchi yetu, kupitia nafasi alizoaminiwa kwa kuchaguliwa na kuteuliwa, kwa moyo wa dhati, uadilifu wa hali ya juu, na uzalendo usiotetereka,” amesema Dk Nchimbi.

Amesema Msuya aliaminiwa kushika dhamana mbalimbali za uongozi katika chama na serikali, ikiwa ni pamoja na kuwa Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM, Makamu wa Kwanza wa Rais na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

“Katika nyadhifa hizo, alionesha uongozi uliotukuka, uliosheheni busara, hekima na kuzingatia maslahi ya wananchi,” amesema.

Amesema anatoa pole kwa familia ya marehemu, ndugu, jamaa, marafiki pamoja na Watanzania wote walioguswa na msiba huo mkubwa kwa Taifa.

Amesema Msuya ataendelea kukumbukwa kama kiongozi aliyeacha alama ya kudumu katika historia ya Tanzania na CCM.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Mawasiliano na Uenezi wa Chadema, Brenda Msuya katika taarifa yake kwa umma, amesema chama chao kimepokea kwa masikitiko makubwa msiba huo.

Brenda amesema Chadema kitamkumbuka Msuya kwa utumishi wake uliotukua kwa Taifa.

“Tutamkumbuka pia kwa kauli yake maarufu aliyosema ndani ya chama chetu kuwa ‘Chadema ni wachambuzi wa mambo’. Kauli iliyobeba heshima na kutambua nafasi ya chama katika mijadala ya leo,” amesema Brenda.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *