Jaji Mruma: Wananchi wengi hawajui kudai haki zao

Morogoro. Kaimu Jaji Mfawidhi Mahakama kuu ya Tanzania kanda ya Morogoro, Amir Mruma amesema wananchi wengi hawajui haki zao katika kupata huduma muhimu ikiwemo umeme na maji.

Amesema hata wanapopata  athari zitokanazo na huduma iliyotolewa kwa uzembe, huchukulia ni hali ya kawaida.

Jaji Mruma amebainisha hayo leo Jumapili, Februari 2, 2025 wakati akifunga maonyesho ya wiki ya sheria yaliyokuwa yakiendelea mkoani humo.

Amesema Mamlaka ya udhibiti wa huduma za nishati na maji (Ewura CC) bado haijatekeleza ipasavyo jukumu lake la msingi la kutoa elimu kwa wananchi, kuhusu namna ya kudai haki zao na kulipwa fidia pindi wanapopata athari zitokanazo na uzembe kwa mamlaka zinazotoa huduma hizo.

Amesema ni wajibu wa Ewura CC kupeleka elimu kwa wananchi kwamba, huduma ya umeme ni biashara.

 “Umeme imetakatwa na unaporudi majokofu matatu yameungua, hujui ufanye nini maisha yanaendelea. Hayo ni mazoea ambayo yanatakiwa yaishe, Bunge lilishaweka sheria ya jinsi ya kudhibiti vitu kama hivyo ni wajibu wenu Ewura CC kupeleka elimu kwa wananchi.”

Ofisa Mwandamizi huduma kwa Wateja (Ewura CC) mkoani Morogoro, Chipegwa Samwel amesema kwa mujibu wa sheria ya huduma ya maji ya mwaka 2020 zimetoa maelekezo kwamba mtu akilipia huduma ya maji anatakiwa aunganishwe ndani ya siku saba za kazi.

Amesema endapo mtu hajaunganishwa na huduma zikifika siku saba anapaswa kulipwa fidia ambapo  kuu inaanzia Sh15,000 na kadri siku zinavyoongezeka fidia nayo ndio inaongezeka kwa Sh5000.

“Mlalamikaji anapotoa lalamiko lake kwa mtoa huduma, kanuni zinamtaka mtoa huduma alishughulikie ndani ya siku tano za kazi, lisiposhughulikiwa kanuni imetoa kiwango cha fidia ambacho ni Sh15,000 na Sh5000 inaongezeka kadri siku lalamiko lake halijafanyiwa kazi, hivyo mwananchi anapaswa kufika Ofisi za Ewura CC kujaza fomu na kuanza mchakato,” amesema Samwel.

Maadhimisho ya sheria na wiki ya sheria huandaliwa na Mahakama Kuu ya Tanzania na  hufanyika Januari kila mwaka na kuhudhuriwa na taasisi mbalimbali zinazojihusisha na masuala ya msaada wa kisheria.

Zaidi ya wananchi 6,250 mkoani Morogoro wamefikiwa ana kwa ana kupatiwa elimu na usuluhishi wa changamoto zao zinazohusu masuala ya sheria, kupitia maonyesho ya wiki hiyo yaliyoanza Januari 25, 2025.