Dar es Salaam. Majaji na mahakimu wanakabiliwa na changamoto nyingi katika utekelezaji wa majukumu yao, hasa kutokana na uzito wa uamuzi wanaopaswa kuutoa.
Mazingira ya utendaji wao wa kazi yanahitaji usawa wa kijinsia na uadilifu wa hali ya juu kama anavyoeleza Jaji wa Mahakama ya Rufani Tanzania, Barke Sehel katika mahojiano na Mwananchi kuelekea Siku ya Kimataifa ya Wanawake Duniani (IWD), Machi 8 na siku ya majaji na mahakimu wanawake duniani inayoadhimishwa Machi 10.
“Kupewa dhamana ya kutoa uamuzi wa haki si jambo dogo, kuna namna ambavyo unapaswa kumtanguliza Mungu akusaidie kutoa uamuzi sahihi, usimnyime mtu haki yake wala usimpendelee mwingine. “Ukichanganya hili na changamoto nyingine za kimaisha tunazopitia wanawake unaweza kuona ni muhimu kiasi gani kwa majaji na mahakimu wanawake kuendelea kukumbushana umuhimu wa kukabiliana na msongo wa mawazo,” anasema Jaji Barke.
Barke ambaye pia ni Mwenyekiti wa Chama cha Majaji na Mahakimu Wanawake Tanzania (TAWJA), anasema miongoni mwa vitu ambavyo chama kinavipa kipaumbele kwa wanachama ni suala la afya ya akili kutokana na uzito wa majukumu waliyonayo, hivyo kuhitaji utulivu mkubwa wa akili.
“Kuwa jaji au hakimu haindoi uhalisia kwamba wewe ni mwanamke, kama tunavyofahamu mwanamke ana majukumu yake kama mama, mke au nafasi yoyote kwenye familia. Katika kujigawa ili kuyatimiza majukumu yote unaweza kujikuta akili yako inazidiwa.
“Kuna wakati unajikuta uko nyumbani lakini kichwa chako kinatawaliwa na mawazo kuhusu kesi fulani unayoisikiliza, huwa inatokea hadi usiku unaota kesi iliyo mezani kwako, dhamana ya kutoa uamuzi wa haki si jambo dogo. Hata unaposikiliza kesi au unaposoma jalada kabla ya kusikiliza kesi unaomba Mungu akuongoze,” anasema.

Jaji Barke anasema katika kipindi alichofanya kazi akiwa jaji ameshughulikia kesi kadhaa zilizoendelea kubaki kichwani mwake hata baada ya kutoa hukumu, ikiwamo ya mauaji ambayo shahidi pekee alikuwa mtoto wa miaka mitano.
“Kesi hii iligusa mno moyo wangu ilikuwa ya mauaji na shahidi pekee alikuwa mtoto mwenye miaka mitano. Ilikuwa ngumu kuona maumivu anayopitia mtoto yule aliyeshuhudia mauaji ya mzazi wake. Namna anavyosimulia na jinsi taswira ile inavyoendelea kuwepo kichwani mwake hadi atakapokua ilinigusa mno.
“Huu ni mfano mmoja lakini haya ndiyo maisha wanayopitia majaji na mahakimu na si wanawake tu, bali hata wanaume. Kwa upande wetu wanawake mambo yanaweza kuwa mengi zaidi ukichanganya na changamoto za familia, hivyo huwa tunakumbushana umuhimu wa kukabiliana na msongo wa mawazo kuepusha hatari inayoweza kujitokeza hali ikiwa mbaya zaidi,” anasema.
Fani ya sheria
Jaji Barke anasema katika kipindi cha miaka 30 tangu kufanyike mkutano wa Beijing, China kuzungumzia masuala ya wanawake, idadi yao kwenye kada ya sheria imeongezeka ikilinganishwa na ilivyokuwa awali.
Wakati huo hakukuwa na jaji mwanamke kwenye Mahakama ya Rufani lakini sasa kuna majaji 13 na Mahakama Kuu kwa sasa kuna majaji wanawake 40.
“Hizi namba angalau zinaonyesha nafasi ya mwanamke kwenye taaluma ya sheria inazidi kuongezeka, tena huko Mahakama Kuu tunaeleka kuwa 50 kwa 50. Tunafurahi zaidi kuna wasichana wanasoma na kuhitimu shahada za sheria.
“Siku hizi watoto wa kike wamekuwa na mwamko wa kusoma na kujiendeleza kielimu katika fani mbalimbali, ikiwamo hii yetu ya sheria na wanafanya vizuri nasi tunazidi kuwatia moyo waje milango iko wazi,” anasema.
Ilikuwaje akasoma sheria
Barke anasema kuwa jaji haikuwa ndoto yake wala ya wazazi wake, siku zote baba yake alitaka awe daktari naye alitamani kuwa balozi.
Anasema mambo yalibadilika baada ya kumaliza kidato cha nne alipochagua masomo ya lugha aliyoyapenda na si sayansi kama alivyotaka baba yake.
“Nilipokuwa mdogo nilitamani kuwa balozi niliamini hiyo ndiyo kazi yenye heshima na niliipenda. Wakati nawaza hivyo, baba yangu alipenda niwe daktari na nilikuwa nafanya vizuri kwenye masomo ya sayansi ila binafsi nilikuwa silipendi somo la biolojia.
“Ilipofika wakati wa kuchagua mchepuo niliweka chaguo la kwanza masomo ya lugha (Kiswahili, Kiingereza na Kifaransa) kisha yakafuata ya sayansi. Hili nililifanya kwa siri, siku niliyomwabia baba alikasirika, matokeo yalipotoka nilifanya vizuri masomo yote ila nikachaguliwa KLF,” anasema.
Huo ndiyo ukawa mwisho wa uhusiano wa Barke na masomo ya sayansi, hata alipomaliza kidato cha sita na kwenda jeshini, anasema alipata hamasa ya kusoma sheria, hivyo akaomba kozi hiyo.
“Nilituma maombi Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) na Chuo Kikuu cha Kentucky cha Uingereza, nilichaguliwa kote lakini nikatamani kwenda kusoma Uingereza, changamoto ikawa fedha. Baba akaniambia hana uwezo wa kunilipia, matumaini ya kwenda huko yakapungua lakini kwa bahati nzuri baba alisikia kuhusu ufadhili unaotolewa na Serikali kwa wanafunzi wanaokwenda nje.
“Nilifuatilia nikatuma maombi na kwa bahati nikawa miongoni mwa waliopata ufadhili. Nilikwenda kusoma, nilipomaliza nikarejea nchini. Kuna kampuni ilitaka kuniajiri baba akasema kama nimesomeshwa na Serikali basi nisiajiriwe kokote lazima nikafanye kazi serikalini,” anasema.
Licha ya kuwa alifahamu kampuni iliyomhitaji ilikuwa na malipo mazuri, anasema alimsikiliza baba yake.
Kituo chake cha kwanza kilikuwa Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) iliyokuwa chini ya Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali ambako aliajiriwa kama wakili wa Serikali akitetea Jamhuri.
Aliendelea na kazi ofisi ya DPP, kisha Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali hadi mwaka 2014 alipoteuliwa kuwa jaji.
Ulinzi haki za wanawake
Barke anasema mfumo wa sheria nchini umeendelea kufanya jitihada kubwa kuhakikisha mwanamke analindwa kisheria, hilo linathibitishwa na sheria mbalimbali zilizoandaliwa kwa kusudi la kuhakikisha ulinzi wa mwanamke na mtoto wa kike.
Anatoa mfano wa Katiba ya nchi inayosisitiza katika usawa, sheria ya ulinzi wa mtoto, sheria ya kuzuia na kupambana na rushwa inayoitaja rushwa ya ngono kama kosa la jinai.
“Ukweli ni kwamba tunapiga hatua licha ya kuwepo maeneo machache ambayo bado, mfano hili la sheria ya ndoa ambayo kwa sasa inatoa mwanya kwa watoto wenye umri chini ya miaka 18 kuingia kwenye ndoa kwa ridhaa ya wazazi. “Mahakama tumeshafanya kazi yetu tumeielekeza Serikali kuifanyia mabadiliko.
“Changamoto nyingine ni zile mila na desturi kandamizi katika baadhi ya jamii ambazo zinamkandamiza mtoto wa kike, hizi zinaweza kubadilishwa kwa jamii kuendelea kuelimishwa ili iondokane na mfumo dume,” anasema.
“Hili la elimu likiwekewa mkazo linaweza kusaidia hata kupunguza vitendo ya ukatili. Miaka ya hivi karibuni tumeshuhudia matukio mengi ya ukatili yanayohusisha vipigo na mauaji dhidi ya wanawake. “Ukifuatilia unakuta chanzo chake ni ugomvi kwenye mapenzi, hapa kuna haja ya elimu kuendelea kutolewa watu wajue kuhimili changamoto zinapotokea na si kuchukua hatua zinazogharimu maisha ya wengine.”
Anasema inapotokea ugomvi kati ya wenza ni vyema wazazi au watu wazima wakae na wahusika kuangalia ukubwa wa mgogoro huo, kama unaweza kutatulika na maisha yakaendelea au vinginevyo.
Siku ya wanawake
Jaji Barke anasema Siku ya Kimataifa ya Wanawake Duniani ni muhimu kutambua mchango wao kwa jamii.
“Ujumbe wangu kwa wanawake na watoto wa kike watambue kuwa inawezekana, wanapaswa kusimama kwenye nafasi zao wafikie malengo waliyojiwekea. Hutakiwi kukata tamaa kwa sababu maisha ni yako, unapaswa kujituma, hakika utafanikiwa.
“Kwa upande wa Serikali, asasi za kiraia, sekta binafsi wote kwa pamoja tunapaswa kutambua suala la usawa wa kijinsia ni letu sote, hivyo tuna jukumu la kuhakikisha linafanikiwa ili tuwe na dunia yenye amani, inayotambua haki na usawa kijinsia,” anasema.