
Dar es Salaam. Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, imemwamuru Inspekta Jenerali wa Polisi (IGP) na Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, kuwaachia huru au kuwafikisha mahakamani watuhumiwa wanne wanaowashikilia.
Amri hiyo imetolewa leo Jumanne Februari 4, 2025 na Jaji David Ngunyale alipotoa uamuzi kufuatia maombi (Habeas Corpus) namba 1386 ya 2025 yaliyofunguliwa na watuhumiwa hao waliokamatwa na polisi kati ya Desemba 24 na 31, 2024.
Tangu wakamatwe huko Mbezi Beach Wilaya ya Kinondoni jijini Dar es Salaam wakituhumiwa kwa wizi, wameendelea kushikiliwa katika Kituo cha Kati bila kufikishwa kortini au kupewa dhamana ya polisi huku ndugu wakizuiwa kuwaona.
Watuhumiwa hao ni Kelvin Mroso, Genes Asenga, Dismas Sunni na Naidha Ngimba waliofungua maombi hayo dhidi ya Mkuu wa Kituo (OCS) cha Kati Jijini Dar es Salaam, IGP, RPC Dar es Salaam kama mdaiwa wa kwanza hadi watatu.
Waliwaunganisha Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP) na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG) na walifungua maombi hayo chini ya hati ya kusikilizwa haraka kupitia kiapo cha Melkisedeck Antony na Valerian Asenga ambao ni ndugu.
Watuhumiwa hao waliwakilishwa na wakili wao, Revocatus Sedede huku upande wa wajibu maombi ambao haukuwasilisha kiapo kinzani hadi maombi hayo yanawasikilizwa, walitetewa na wakili wa Serikali, Edith Mauya.
Jaji Ngunyale amesema kwa kuwa, wajibu maombi hawakuwasilisha kiapo cha majibu kinzani kama ilivyotakiwa kisheria, hiyo inawazuia wajibu maombi kufanya mawasilisho ya masuala ya ukweli kwa kuwa inachukuliwa wanakubali.
Hoja ya watuhumiwa
Akiwasilisha hoja kuhusiana na maombi hayo, wakili Revocatus aliegemea kile kilichoelezwa na ndugu wa watuhumiwa katika kiapo chao na kusisitiza kuwa, wamefanya kila jitihada ili watuhumiwa wapate dhamana bila mafanikio.
Wakili alieleza kuwa, polisi wamezuia dhamana bila uwepo wa sababu yenye mashiko zaidi ya kueleza kuwa ni hadi upelelezi ukamilike jambo ambalo linakiuka haki chini ya kifungu 32(1) cha sheria ya mwenendo wa makossa ya Jinai (CPA).
Aliongeza kuwa, Ibara ya 15(1) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 imevunjwa kutokana na polisi kuwanyima dhamana au kuwapeleka mahakamani ndani ya saa 24 tangu walipokamatwa na polisi.
Jaji amesema wasilisho la wakili Mauya halikuzingatiwa na Mahakama hiyo kwa kuwa alifanya wasilisho kuhusu mambo ya ukweli (matters of fact) kinyume cha sheria na katika wasilisho lake, hakuwasilisha hoja yoyote ya kisheria kupinga.
Uamuzi wa Jaji
Jaji Ngunyale amesema amepitia kwa umakini hati za kuitwa shaurini na hati ya viapo pamoja na mawasilisho na hoja inayopaswa kuamuliwa na Mahakama yake kama waombaji wana uthibitisho wa kutosha wa kile wanachokiomba.
Kwa mujibu wa Jaji, Mahakama imeridhika na uhalali wa kile kinachoombwa na watuhumiwa hao ambacho ni kuachiwa huru lakini ili kutoa amri, ni lazima ajiridhishe kuwa walikamatwa au kuwekwa mahabusu kinyume cha sheria.
Jaji amesema ni jambo lisilobishaniwa, waombaji walikamatwa na polisi na kuwekwa mahabusu kituo cha kati jijini Dar es Salaam kati ya Desemba 24 na 31,2024 na hadi jana wakati wakati maombi yao yakisikilizwa, bado wanashikiliwa.
“Kimsingi hakuna ubaya katika ukamataji wa washukiwa lakini hata hivyo, wajibu maombi walipaswa kufuata misingi ya kisheria baada ya kuwakamata ikiwamo kuwaachia kwa dhamana ya polisi au kuwapeleka mahakamani,”amesema.
Jaji amesema katika maombi yaliyoko mbele yake, waombaji bado wanashikiliwa katika mahabusu ya polisi nje ya muda wa saa 24 uliowekwa na sheria tangu walipokamatwa na polisi, hivyo kufanya jambo hilo kuwa haramu kisheria.
Kwa mujibu wa Jaji, watuhumiwa wako mikononi mwa polisi tangu walipokamatwa zaidi ya saa 24 za muda uliowekwa na sheria na anaona kitendo cha kuendelea kuwashikilia kwa muda mrefu ni kukiuka haki na ni kinyume cha sheria.
Jaji akaamuru:“Ninaagiza Kelvin Mrosso, Genes Asenga, Dismas Sunni na Naidha Ngimba waachiliwe kutoka mahabusu ya polisi.”