
Dodoma. Waziri wa Viwanda na Biashara, Selemani Jafo amewataka Watanzania kupunguza matumizi ya pombe kali, akisema kuwa ni hatari kwa afya zao.
Jafo ametoa kauli hiyo leo Alhamisi Mei 15, 2025 jijini Dodoma alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari kuhusu mafanikio ya wizara hiyo kwa kipindi cha miaka minne ya Serikali ya awamu ya sita.
Ameeleza kuwa hivi karibuni kumekuwa na malalamiko kuhusu uingizaji wa pombe feki hasa vikali, kufuatilia taarifa hiyo Serikali iliunda kamati maalumu kutoka sekta za viwanda, biashara, kilimo na mifugo kwa ajili ya kuchunguza kwa kina suala hilo.
Amesema kuwa ripoti ya kamati hiyo imebainisha kuwa pombe zote zinazozalishwa ndani na zile zinazoingizwa nchini hukaguliwa na kuthibitishwa na Shirika la Viwango Tanzania (TBS), hivyo hakuna ushahidi wa uwepo wa pombe bandia.
Jafo amefafanua kuwa changamoto kubwa iliyojitokeza ni unywaji uliokithiri miongoni mwa baadhi ya watumiaji, na akatoa wito kwa Watanzania kunywa kwa kiasi ili kulinda afya zao.
“Hakuna pombe bandia, kilichobainika ni unywaji wa pombe uliopitiliza. Watu wanachanganya pombe kali, na hii ni hatari. Naishauri jamii kunywa kwa kiasi,” amesema Jafo.
Pia, Waziri Jafo amezungumzia mafanikio ya sekta ya viwanda, akibainisha kuwa Serikali imezalisha sukari ya kutosha kwa matumizi ya viwanda vya ndani.
Mahitaji ya sukari ya majumbani ni tani 552,000, lakini uwezo wa viwanda vya ndani kuzalisha sukari ni tani 631,000 ikiwa vitafanya kazi kwa kiwango cha juu.
Hata hivyo, ameeleza kuwa uzalishaji wa sukari unakabiliwa na changamoto mbalimbali, ikiwemo mvua kubwa ambazo husababisha madhara katika mashamba ya miwa.
Amesema kuwa mwaka jana, kiwanda cha Kilombero kilizalisha chini ya kiwango cha kawaida kutokana na mvua kubwa, na uzalishaji ulifika tani 416,000 pekee.
Jafo amesema kuwa uagizaji wa sukari kutoka nje ya nchi ulileta athari kubwa kwa viwanda vya ndani, kwani ulilenga kuvunja viwanda hivyo na kuhatarisha ajira za Watanzania waliokuwa wakifanya kazi katika mnyororo wa thamani wa sukari.
Kwa upande mwingine, Jafo amesema Serikali inaendelea kufanya sensa ya viwanda vilivyokufa ili kuchukua hatua za kuvifufua.
Amebainisha kuwa viwanda vya zamani, takribani 9,048 vikifufuliwa vitatoa ajira milioni sita, ambapo ajira milioni 1.4 zitakuwa za moja kwa moja na kuwanufaisha Watanzania.
Jafo amesema Serikali inaendelea na ukarabati wa viwanda vilivyoshindwa kufanya kazi kwa muda mrefu ili vianze tena kuzalisha na kutoa ajira kwa Watanzania.