Jafo aunda kamati kuchunguza biashara za wageni Tanzania

Dar es Salaam. Zikiwa zimepita siku tatu tangu Rais Samia Suluhu Hassan atoe agizo kwa Waziri wa Viwanda na Biashara, Dk Selemani Jafo kuangalia wageni wanaofanya biashara zinazofanywa na wenyeji, waziri ameunda kamati ya watu 15.

Rais Samia alitoa agizo hilo Januari 30, 2025, Ikulu jijini Dar es Salaam wakati wa halfa ya chakula cha mchana alichokiandaa kwa ajili ya washiriki wa shughuli ya uokoaji wa kuporomoka kwa jengo Kariakoo.

Katika tukio hilo, watu 31 walipoteza maisha, zaidi ya 80 wakijeruhiwa huku mali na miundombinu ikiharibika na kupotea.

“Waziri wa biashara naomba ukaliangalie vyema suala la wageni kufanya biashara zinazofanywa na wenyeji, niliwahi kurushiwa clip ya Kariakoo mgeni anapigana na wenyeji nikauliza kwa nini wanapigana wakasema yule ni mmachinga. Haiwezekani mgeni akawa mmachinga je vijana wetu watafanya shughuli gani,” alihoji.

Eneo lingine alilozungumzia Rais Samia ni kukosekana kwa ushindani wa kibiashara kati ya wafanyabiashara wazawa na wale wanaotoka nje ya nchi, kilio kilichowasilishwa na Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wafanyabiashara wa Kariakoo, Severine Mushi.

Kumekuwa na malalamiko ya ongezeko la raia wa kigeni wanaofanya biashara za rejareja (machinga), hali inayowaathiri wafanyabiashara wazawa katika Soko la Kariakoo.

Mushi alisema kwa sasa wanakabiliana na ushindani mkubwa na wafanyabiashara wa kigeni hali inayotishia ustawi wa biashara za wazawa katika eneo hilo la Kariakoo.

Akijibu hilo Rais Samia alisema:“Nimeelekeza Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kutopendelea wafanyabiashara wote walipe kodi na wawe na usawa katika soko.”

Leo Jumapili, Februari 2, 2025, Waziri Jafo akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam ametangaza hatua ya kuunda kamati hiyo itakayofanya kazi kwa siku 30 ikiongozwa na Mkuu wa Chuo cha Elimu ya Biashara (CBE), Edda Lwoga.

Amesema lengo la kamati hiyo ni kufanya uchunguzi wa kina kuhusu biashara za wageni nchini, kuchambua vibali na leseni wanazopatiwa na kubaini maeneo yenye changamoto kubwa.

“Kamati hiyo itachunguza jinsi wageni wanavyopata vibali vya biashara, uhalali wa leseni zao na sababu zinazosababisha wawekezaji hao kujihusisha na biashara zisizo za uwekezaji,” amesema Jafo.

Amesema kamati hiyo pia, itafanyia uchunguzi wa nyumba za wageni na biashara wanazofanya, pamoja na njia wanazotumia kuepuka taratibu rasmi za biashara.

“Hili linawaathiri vijana wetu na wafanyabiashara wazawa, kwani inaathiri mitaji yao, wengine wanafilisika na kushindwa kurejesha mikopo ya benki,” amesema.

Pia, amesema baadhi ya wageni wanamiliki maghala makubwa na kushiriki biashara za rejareja, jambo linaloathiri mapato ya Serikali kupitia kodi.

Jafo amesema tatizo hilo si Kariakoo pekee, bali lipo pia katika sekta nyingine kama madini.