
Usafiri wa pikipiki maarufu bodaboda umeleta unafuu mkubwa wa usafiri katika miji mingi mikubwa nchini, hususan maeneo yenye msongamano mkubwa wa magari.
Hata hivyo, changamoto kubwa inayojitokeza ni matumizi ya bodaboda katika vitendo vya uhalifu, hasa uporaji wa simu, pochi, na mizigo ya wananchi.
Matukio hayo yanazua hofu miongoni mwa wakazi wa miji mbalimbali kama Dar es Salaam, Arusha, Mwanza, Mbeya, Dodoma, na Tanga, huku yakichafua sifa ya madereva wengi wa bodaboda wanaofanya kazi kwa uaminifu.
Takwimu na ushuhuda wa wananchi wanaoathirika na vitendo hivi vinaonyesha kuwa baadhi ya wahalifu wanaojulikana ‘vishandu’ wanatumia pikipiki kukwapua mali za watu na kutokomea kwa kasi.
Matukio hayo yameripotiwa katika baadhi ya maeneo ndani ya Dar es Salaam kama Kinondoni, Kariakoo, Ilala, Temeke, Mwenge, na pia katika miji mingine mikubwa nchini. Mbinu zinazotumiwa na wahalifu hawa ni za ghafla na mara nyingi huacha waathirika wakiwa hawana msaada wowote wa kuwapata wahusika.
Hata hivyo, ni dhahiri kuwa si madereva wote wa bodaboda wanaojihusisha na vitendo hivi vya kihalifu. Kwa mujibu wa viongozi wa vyama vya waendesha bodaboda, ni kundi dogo la watu wachache linalochafua taswira ya waendesha bodaboda kwa ujumla.
Ni dhahiri juhudi za haraka zinatakiwa kuchukuliwa ili kuhakikisha waendesha bodaboda waaminifu hawaathiriki na vitendo vya wachache.
Katika kukabiliana na tatizo hilo, hatua mbalimbali zichukuliwe, kwanza kunapaswa kuwapo kwa ushirikiano wa karibu kati ya waendesha bodaboda na vyombo vya usalama. Viongozi wa vyama vya bodaboda wanatakiwa kuwahamasisha wanachama wao kushirikiana na polisi katika kuwabaini wahalifu. Pia madereva wa bodaboda waaminifu wantakiwa kuwa tayari kutoa taarifa kwa polisi wanaposhuhudia au kuwa na mashaka juu ya mwenendo wa wenzao.
Pili, Serikali na vyombo vya usalama viimarishe mikakati ya kudhibiti uhalifu huo. Polisi watumie napaswa kutumia mbinu za kisasa kama kamera za usalama na upelelezi wa kisayansi ili kuwabaini wahalifu hawa kwa haraka.
Aidha, hatua za kudhibiti soko la bidhaa za wizi, hasa simu za mkononi, zinapaswa kupewa kipaumbele.
Ili kukabili changamoto hiyo, bodaboda zinapaswa kusajiliwa na kuwa na utambulisho wa wazi, kama namba za usajili na sare maalumu za madereva.
Hii itasaidia kupunguza uhalifu unaofanywa na waendesha bodaboda wasio na utambulisho rasmi. Pia, ukaguzi wa mara kwa mara wa bodaboda unapaswa kufanyika ili kuhakikisha zinatumika kwa shughuli halali pekee.
Pamoja na hayo, tunatoa wito kwa jamii kuwa macho na kutoa taarifa haraka polisi pale wanaposhuhudia vitendo vya uhalifu. Pia wananchi wachukue tahadhari wanapotembea mitaani, hasa katika maeneo yenye matukio mengi ya uporaji.
Tunaamini Serikali, polisi, waendesha bodaboda, na wananchi wakishirikiana wanaweza kufanikisha kukomesha uhalifu huo, kwani ni jukumu la kila mmoja kuhakikisha miji yetu inakuwa mahali salama kwa wakazi wake wote.