Dec 12, 2024 06:29 UTC
Televisheni ya Al-Jazeera ya Qatar imetangaza leo Alkhamisi kwamba Wapalestina 42 wameuawa shahidi na makumi ya wengine kujeruhiwa katika mashambulizi ya alfajiri ya leo yaliyofanywa na utawala wa Kizayuni kwenye Ukanda wa Ghaza.
Kwa mujibu wa shirika la habari la Fars; Vyombo vya habari vya Palestina vimeripoti habari za kuendelea jinai za jeshi la Kizayuni katika maeneo tofauti ya Ukanda wa Ghaza Alkhamisi asubuhi.
Katika ripoti yake, Al-Jazeera imetangaza kuwa, ndege za utawala wa Kizayuni unaozikalia kwa mabavu ardhi za Palestina zimeshambulia ghorofa moja la makazi ya raia katika mtaa wa Al-Jalaa wa magharibi mwa Mji wa Ghaza na kuua shahidi Wapalestina 7 na kujeruhi wengine wengi.
Ripoti hiyo imeongeza kuwa, shambulio jingine la jeshi katili la Israel kwenye viunga vya Rafah kusini mwa Ukanda wa Ghaza limeua shahidi Wapalestina wanane na kujeruhi wengine 30.
Mwandishi wa televisheni ya Al Jazeera katika Ukanda wa Ghaza aidha amesema: Wapalestina wengine 12 wameuawa shahidi mapema leo Alkhamisi na makumi ya wengine wamejeruhiwa baada ya jeshi dhalimu la Israel kushambulia kikatili kituo cha misaada ya kibinadamu magharibi mwa mji wa Ghaza.
Ripoti hiyo imeongeza kuwa, “Wapalestina 15 wengine wameuawa shahidi katika mashambulizi mawili ya wanajeshi vamizi wa Israel kwenye mtaa wa al-Rashid wa kusini mwa Ukanda wa Ghaza.”