Dec 12, 2024 06:31 UTC
Mashirika ya habari ya nchi za Magharibi yameakisi kwa wingi hotuba na miongozo muhimu ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu aliyotoa jana Jumano akisisitiza kuwa Marekani na utawala wa Kizayuni ni wahusika wakuu wa matukio ya Syria.
Shirika la habari la Reuters la utawala wa kifalme wa Uingereza limeandika: (Ayatullah) Ali Khamenei Jumatano amesema, Iran ina ushahidi unaoonesha kuwa, kupinduliwa serikali ya Rais Assad wa Syria ni njama za Marekani na Israel na mmoja wa majirani wa Syria lakini hakutaja ni jirani gani huyo.
Shirika hilo la habari limeendelea kuandika: Uturuki ambayo ni mwanachama wa NATO, ilikuwa inazikalia ardhi za kaskazini mwa Syria baada ya kufanya mashambulizi kadhaa dhidi ya wanamgambo wa Kikurdi na (Erdogan) alikuwa mmoja wa waungaji mkono wakuu wa wapinzani wa Bashar al Assad tangu baada ya kuanza vita vya ndani ya Syria mwaka 2011.
Gazeti la Associated Press la nchini Marekani nalo limeandika: Ayatullah Khamenei, Kiongozi Mkuu wa Iran amesema kuwa matukio ya hivi karibuni ya Syria ikiwa ni pamoja na kuanguka serikali ya nchi hiyo ni njama ya pamoja ya Marekani na Israel.
Gazeti la AFP la Ufaransa nalo limeandika: (Imam) Khamenei amesema katika hotuba yake ya kwanza tangu kuanguka serikali ya Syria kwamba wako watu wasiojua kitu wanajidanganya wanapodhani kuwa kambi ya Muqawama imedhoofika kwa kuanguka serikali ya Bashar al Assad huko Syria, wanajidanganya pia kudhani kuwa Iran imedhoofika. Watambue kwamba Iran ni imara na itakuwa imara zaidi na Muqawama utaenea zaidi katika eneo hili.