Chanzo cha picha, Getty Images
Ujerumani imesema “haitakubali” na kwamba Ulaya lazima “ijibu kwa uthabiti” huku Rais wa Marekani Donald Trump akilenga magari na vipuri vya magari kutoka nje kwa ushuru wa 25% katika hatua yake ya hivi karibuni.
Mataifa mengine makubwa ya kiuchumi duniani yameapa kulipiza kisasi, huku Ufaransa ikitaja hatua hiyo kuwa “habari mbaya”, Canada ikiita “mashambulizi ya moja kwa moja”, na China ikiishutumu Washington kwa kukiuka sheria za biashara za kimataifa.
Mapema siku ya Alhamisi, hisa za Frankfurt za kampuni za Porsche, Mercedes na BMW zilishuka pamoja na kampuni ya Ufaransa ya Stellantis, waundaji wa Jeep, Peugeot na Fiat.
Trump ametishia kuweka ushuru “mkubwa zaidi” ikiwa Ulaya itashirikiana na Canada kufanya kile anachoelezea kama “madhara ya kiuchumi” kwa Marekani.