Tanzania yapiga marufuku bidhaa zote za kilimo kutoka Afrika Kusini na Malawi

fv

Chanzo cha picha, KL

Maelezo ya picha, Waziri wa Kilimo wa Tanzania, Hussein Bashe

Tanzania
imepiga marufuku rasmi bidhaa zote za kilimo kutoka Afrika Kusini na Malawi, kufuatia
maamuzi ya awali ya nchi hizo mbili wa kupiga marufuku uingizaji wa mazao ya
Tanzania.

Waziri
wa Kilimo wa Tanzania, Hussein Bashe amesema mazungumzo yanaendelea kupitia
Wizara ya Mambo ya Nje, lakini Tanzania haiwezi kuendelea kunyimwa haki ya
kuuza bidhaa zake katika nchi hizo mbili.

Katika
hatua hii ya kulipiza kisasi, Bashe ametangaza kusitisha mara moja uagizaji wa
tufaha za Afrika Kusini na matunda mengine yote.

“Hatutaruhusu
mazao yoyote ya kilimo kutoka Afrika Kusini kuingia katika nchi yetu,” amesema
Bashe.

Waziri
pia ametangaza kupiga marufuku uagizaji wa bidhaa zote za kilimo kutoka Malawi,
na marufuku hiyo itaanza mara moja.

“Kwa
mataifa yote haya – lakini hasa Malawi – hatutaruhusu mazao yoyote ya kilimo kutoka
Malawi kupitia Tanzania,” amesema Bashe.

Zaidi
ya hayo, Waziri huyo amesitisha upelekaji wa mahindi ambayo yalikuwa
yamenunuliwa na Malawi ili kukabiliana na uhaba wa chakula.

“Kuanzia
Mei 1, Malawi ilitarajiwa kuanza kusafirisha mbolea kutoka Tanzania kwa ajili
ya msimu wao wa kilimo. Hatutaruhusu aina yoyote ya mbolea kusafirishwa kwenda
Malawi,” amesema Bashe.

Waziri
huyo ameuhakikishia umma kuwa hatua hizi hazitatishia usalama wa chakula wa
Tanzania.

“Hakuna
Mtanzania atakayekufa kwa kukosa zabibu au tufaha kutoka Afrika Kusini. Kwa
hiyo, tunachukua hatua hizi kulinda maslahi ya Watanzania. Hii ni biashara, na
lazima tuheshimiane,” amesema Bashe.