Polisi yatawanya maandano ya kupinga mauwaji ya Ojwang Kenya

Polisi yatawanya maandano ya kupinga mauwaji ya Ojwang Kenya

Waandamanaji katika jiji la Nairobi walijipata wakikimbilia usalama wao baada ya maafisa wa polisi kuwarushia mabomu ya kutoa machozi.

Waaandamanaji hao, wengi wao vijana walikuwa wanapanga kufanya maombi kumkumbuka Albert Ojwang kabla ya kufanya maandamano ya amani hadi bustani ya Freedom Corner.

Maandamanao yao yanajiri siku moja tu baada ya Naibu Inspekta wa polisi Eliud Lagat kuachia Madaraka kwa muda ili kutoa nafasi kwa uchunguzi wa kifo cha kutatanisha cha Ojwang. Kupitia taarifa iliyotolewa Jumatatu, Lagat alisema kuwa uamuzi wake umechukuliwa “kwa fikra pana na dhamira ya dhati” kutokana na uzito wa ofisi yake na maslahi ya umma kuhusiana na suala hilo.

Taarifa hiyo ilisema na ninanukuu, “Nimeamua kujiweka kando kutoka ofisi ya Naibu Inspekta Jenerali – Huduma ya Polisi Kenya hadi pale uchunguzi utakapokamilika,”  alisema Lagat. “Majukumu ya ofisi sasa yataendeshwa na naibu wangu hadi uchunguzi utakapoisha.”  Taarifa hiyo imeongeza kusema, “Niko tayari kutoa usaidizi wowote utakaohitajika wakati wa uchunguzi wa tukio hili la kusikitisha,” aliongeza. Lakini sasa waandamanaji wanataka ajiuzulu rasmi kwenye wadhfa huo.

Wakati uchunguzi ukiendelea, afisa mkuu wa polisi wa Kituo Kikuu cha Polisi Nairobi, Samson Talaam, na Konstebo wa Polisi James Mukhwana tayari wamekamatwa.

Mamlaka Huru ya Uangalizi wa Polisi (IPOA) pia imewakamata wafungwa raia watatu — Gin Ammitou Abwao, Collins Karani Ireri, na Brian Mwaniki Njue — waliokuwa wakizuiliwa katika kituo hicho hicho wakati wa kizuizi cha Ojwang’.

Kamati ya bunge kuwasilisha ripoti yake

Waandamanaji waliokuwa na mabango wanamtaka Naibu Inspekta wa Polisi Eliud lagat kujiuzulu kufuatia kifo cha kutatanisha cha mwanablogu Albert Ojwang
Waandamanaji waliokuwa na mabango wanamtaka Naibu Inspekta wa Polisi Eliud lagat kujiuzulu kufuatia kifo cha kutatanisha cha mwanablogu Albert OjwangPicha: Gerald Anderson/Anadolu/IMAGO

Mamlaka zinadai kuwa watatu hao walitumiwa na polisi kumtesa Ojwang’, jambo lililosababisha kifo chake. Aidha waandamanaji wanamtaka Waziri wa usalama wa taifa Kipchumba Murkomen ajiuzulu.

Kifo cha Ojwang’ kimezua ghadhabu kote nchini, huku wito wa uwajibikaji kwa maafisa wa juu wa polisi ukiongezeka. Mwanablogu huyo alikamatwa muda mfupi baada ya kuchapisha tuhuma za ufisadi dhidi ya Lagat, hasa kuhusu upangaji wa kimkakati wa maafisa ndani ya Idara ya Upelelezi wa Jinai (DCI) na vitengo vya trafiki, nafasi zinazohusishwa na udhibiti wa mapato na taarifa za kijasusi. Inspekta

Jenerali wa Polisi Douglas Kanja, alipokuwa akihutubia Seneti tarehe 11 Juni, alithibitisha kuwa uchunguzi ulianzishwa kufuatia machapisho ya mtandaoni yaliyosambaa na kumhusisha Lagat na sakata ya ununuzi wa mali ya thamani ya dola milioni 2.6 huko Dubai.

Kifo cha mwanablogu Kenya chamliza mzazi, ataka haki

To view this video please enable JavaScript, and consider upgrading to a web browser that supports HTML5 video

Kifo cha Ojwang’ akiwa mikononi mwa polisi kimeibua upya wasiwasi kuhusu ukiukwaji wa haki, matumizi mabaya ya madaraka, na haja ya dharura ya kuleta mageuzi ya taasisi katika vyombo vya usalama nchini Kenya.

Wakati huo huo, Kamati ya Bunge la Kitaifa ya Idara ya Utawala na Usalama wa Ndani inatarajiwa kuwasilisha ripoti yake inayosubiriwa kwa hamu, ikieleza matokeo ya uchunguzi kuhusu kifo tata cha Albert Ojwang, mwalimu mwenye umri wa miaka 26 aliyeaga dunia katika mazingira yasiyoeleweka akiwa kizuizini katika Kituo Kikuu cha Polisi cha Nairobi.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *