Polisi aliyempiga risasi muuzaji barakoa Nairobi akamatwa

“Kufuatia tukio hilo, Inspekta Jenerali wa Huduma ya Kitaifa ya Polisi ameagiza kukamatwa kwa afisa aliyehusika, kuanzishwa kwa uchunguzi wa haraka, na kufikishwa kwake mahakamani. Afisa huyo tayari amekamatwa,” ripoti hio ilisema .

Maandamano hayo, ambayo yalikuwa na lengo la kushinikiza kujiuzulu kwa Naibu Inspekta Jenerali wa Polisi, Eliud Lagat, yaligeuka na kuwa ya vurugu baada ya makundi ya wahuni kuwavamia waandamanaji.

Ripoti hiyo pia ilibainisha kuwa muathiriwa wa tukio hilo alipelekwa hospitalini ambapo anaendelea kupokea matibabu.

Katika mojawapo ya video zilizosambaa mtandaoni na kuibua taharuki miongoni mwa wananchi, maafisa wawili wa kikosi cha kupambana na ghasia walionekana wakimkamata muuzaji huyo wa barakoa, kumshambulia, na hatimaye kumpiga risasi.

Ripoti zinaonyesha kuwa magenge ya watu waliokuwa wamejihami waliwashambulia waandamanaji kwa kuwapiga na kuwaibia, hali iliyochangia machafuko hayo kuenea.

Taarifa ya polisi ililaani vikali vitendo hivyo vya kihalifu na kusisitiza kuwa watu wote waliotenda uhalifu wakati wa maandamano hayo watachukuliwa hatua kali za kisheria.

“Watu wanaojihusisha na vitendo vya kihuni watakabiliwa kwa uthabiti kwa mujibu wa sheria. Uchunguzi wa kina umeanzishwa ili kuwabaini na kuwachukulia hatua za kisheria wanaohusika,” taarifa hiyo iliendelea.

Inayohusiana

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *