‘Nimefanyiwa upasuaji mara 100 na siachi’ – upasuaji wa urembo wavuma China

..

Maelezo ya picha, Abby Wu, ambaye amefanyiwa upasuaji zaidi ya 100, ni mmoja wa waathiriwa wa kwanza wa upasuaji wa urembo wa China.

  • Author, Natalia Zuo
  • Nafasi, BBC Eye
  • 23 Aprili 2025, 14:58 EAT

    Imeboreshwa Dakika 31 zilizopita

Abby Wu alikuwa na umri wa miaka 14 tu alipofanyiwa upasuaji wa urembo bandia kwa mara ya kwanza.

Baada ya kupata matibabu ya homoni, uzito wa mwili wa Abby uliongezeka kutoka kilo 42 hadi kilo 62 ndani ya miezi miwili.

Mwalimu wake wa michezo ya kuigiza aligundua mabadiliko hayo ya mwili.

Mwalimu wangu aliniambia, ”ulikuwa nyota lakini sasa umekuwa mnene kupita kiasi. Chagua moja uondoke kwa tasnia hii au upunguze kilo,” anakumbuka alichoambiwa kipindi hicho akisubiri kufanya mtihani wake wa tamthilia.

Mama yake Abby aliingilia kati na kuamua kumpeleka kufanyiwa upasuaji wa kuondoa mafuta tumboni na miguuni.

Abby anavuta kumbukumbu jinsi mamake alivyompa motisha akisubiri kufanyiwa operesheni hiyo.

”Kuwa mkakamavu na uingie ufanyiwe. Ukitoka hapo utakuwa mrembo zaidi.”

Upasuaji huo ulimuacha na makovu. Abby alipatiwa dawa za kupunguza uchungu lakini alikuwa macho akifanyiwa operesheni hiyo.

”Ningeona kiasi cha mafuta kilichotolewa mwilini mwangu na damu iliyokuwa ikinivuja,” anasema.

Pia unaweza kusoma

Msichana aliyevalia nguo za kuogelea akiwa amesimama karibu na ufuo wa bahari

Chanzo cha picha, Family handout

Maelezo ya picha, Picha ya Abby kabla y akufanyiwa upasuaji wa urembo akiwa na miaka 14

“Upasuaji ulifanya kazi. Nilijiamini na kuwa na furaha zaidi, siku baada ya siku. Nadhani mama yangu alifanya chaguo sahihi.”

Sasa Abby ana umri wa miaka 35 na amefanyiwa upasuaji wa urembo mara mia moja ikimgharimu dola nusu milioni.

Anamiliki kliniki ya ulimbwende katikati mwa mji wa Beijing na amekuwa mtu tajika katika tasnia ya upasuaji wa plastiki nchini China.

Lakini upasuaji huo pia unaathari zake kwa mwili.

Akiwa amekaa mbele ya kioo anajipodoa ili kuficha makovu ya sindano za kupunguza unene usoni, utaratibu anaoufanya kila mwezi ili kuhakikisha uchanga usoni mwake nakuhakikisha hana ngozi zilizolegea baada ya upasuaji wa kupunguza taya uliondoa mifupa mingi.

Lakini anasisitiza kuwa hajutii upasuaji wa urembo aliyofanya kufikia sasa akiamini kuwa mamake hakukosea kumuanzisha katika ulimbwende huu.

”Upasuaji huu ulikuwa na ufanisi, nilianza kuwa mjasiri na mwenye furaha kila uchao,”anasema Abby

Picha ya mwanamke aliyefungwa bandeji puani na pia usoni.

Chanzo cha picha, Abby Wu

Maelezo ya picha, Abby huelezea safari yake ya upasuaji wa urembo katika mitandao ya kijamii, akionyesha uhalisia baada ya kufanyiwa operesheni

Awali ikionekana kama ni mwiko, upasuaji wa plastiki umevuma kwa zaidi ya miaka 20 nchini China ikichochewa zaidi na mitazamo ya kijamii haswa inayoendekezwa mitandaoni.

Ingawa mwonekano wa nje daima umekuwa na umuhimu mkubwa katika utamaduni wa Kichina, hasa kwa wanawake, viwango vya uzuri nchini humo vinaendelea kubadilika.

Kwa muda mrefu, sifa zilizopendekezwa zaidi zilikuwa mchanganyiko wa maadili ya uzuri wa Magharibi, taswira za kubuni kutoka katuni za Kijapani (anime), na mvuto wa mtindo wa K-Pop: kope za mara mbili, taya iliyochongwa kwa ustadi, pua iliyo wazi na yenye umbo la kuvutia, pamoja na uso wa mlingano mkamilifu

Hata hivyo, siku hizi, taratibu za urembo zinazotia wasiwasi zimeanza kushika kasi zikilenga kufanikisha taswira isiyo halisi ya uzuri wa kike uliopitiliza, unaokaribia sura ya mtoto.

Sindano za kuondoa mikunjo zinazofahamika kama Botox sasa hupigwa nyuma ya masikio ili kuyasukuma mbele, jambo linaloleta taswira ya uso mdogo na mwororo.

Upasuaji wa kope za chini, ukichochewa na mwonekano wa macho yenye mwanga mwingi wa mashujaa wa katuni, hupanua macho kwa lengo la kuwasilisha sura ya kitoto isiyo na hatia.

Kufupishwa kwa mdomo wa juu kati ya pua na mdomo wa juu kunaaminika kuashiria ujana na mvuto wa ujana.

Hata hivyo, uzuri huu mara nyingi huundwa kwa ajili ya kamera.

Chini ya vichujio vya picha na mwanga, matokeo huweza kuonekana kuwa ya kuvutia bila dosari.

Lakini katika maisha halisi, athari yake huwa ya kushangaza sura isiyo ya kibinadamu kikamilifu, wala ya kitoto kikamilifu.

.

Chanzo cha picha, TikTok

Maelezo ya picha, Viwango vya urembo wenye sumu vinashirikiwa kwenye mitandao ya kijamii nchini Uchina, na kupotosha kile kinachoonekana kuwa cha kawaida

.

Chanzo cha picha, SoYoung

Maelezo ya picha, Tangazo la programu ya upasuaji wa vipodozi ya SoYoung’s lilisema “mwanamke hukamilika tu anapokuwa mrembo”

Programu za upasuaji wa urembo kama SoYoung (New Oxygen) na GengMei (More Beautiful) zimekuwa zikipata umaarufu mkubwa, zikitangaza kuwa na uwezo wa kuchanganua “dosari za uso” kwa kutumia algorithimu za kisasa.

Baada ya kuchanganua sura ya mtumiaji, programu hizi hutoa mapendekezo ya upasuaji kutoka kwa kliniki zilizo karibu, na hupata kamisheni kwa kila huduma inayotolewa.

Mwelekeo huu wa urembo, pamoja na mitindo mingine, umechochewa kwa kasi kupitia mitandao ya kijamii, ukishirikiwa na kutangazwa na watu mashuhuri na waathiri, na hivyo kubadilisha kwa haraka vigezo vya kile kinachochukuliwa kuwa uzuri au hali ya kawaida.

Abby, mmoja wa waathiri wa mwanzo kabisa wa upasuaji wa urembo nchini China, ameweka wazi safari yake kupitia video na picha katika majukwaa mbalimbali ya kijamii.

Alijiunga na SoYoung punde tu baada ya kuzinduliwa, na tangu wakati huo amefanyiwa zaidi ya upasuaji100 wa urembo.

Hata hivyo, anapotumia programu hiyo kuchanganua sura yake, bado huonyeshwa kasoro kadhaa pamoja na orodha ndefu ya mapendekezo ya upasuaji.

“Inasema nimefura chini ya macho. Nipate upanuzi wa kidevu? Tayari nimefanya huo,” Abby asema kwa kicheko. “Kupunguza pua? Je, nifanye upasuaji mwingine wa pua tena?”

Tofauti na majukwaa ya kawaida ya biashara mtandaoni, programu kama SoYoung zimegeuka kuwa mitandao ya kijamii ya urembo.

Watumiaji hushiriki kumbukumbu za kina kabla na baada ya upasuaji, na mara nyingi huomba ushauri kutoka kwa watumiaji mahiri kama Abby.

‘Ngozi yangu ilihisi kama kuna simiti chini yake’

Changamoto ni kuafiki mahitaji ya kliniki ambazo zimechipuka kote China kuna uhaba wa madaktari hitimu na kliniki zisizo na leseni.

Ripoti ya iResearch ya 2019 ilibaini kuwa kulikuwa na maeneo 80,000 yaliyokuwa yakitoa huduma bila leseni, na wahudumu 100,000 bila sifa zinazohitajika.

Inakadiriwa kuwa mamia ya ajali hutokea kila siku kwenye kliniki hizo kutokana na huduma duni.

Dkt. Yang Lu, mmiliki wa kliniki yenye leseni, anasema watu wengi wanamjia kurekebishiwa upasuaji uliofanyika vibaya.

Baadhi ya wagonjwa walifanyiwa upasuaji katika nyumba za watu binafsi, jambo linalozua hatari zaidi.

.

Maelezo ya picha, Yue Yue (kulia), kwa kushauriana na Dk Yang, anasema upasuaji wake ambao haujakamilika umeathiri kazi yake katika kitengo cha HR.

‘iliharibu ajira yangu’

Kila mwaka, maelfu ya watu kama Yue Yue huangukia katika mikono ya kliniki za urembo zisizo na leseni nchini China.

Hata hivyo, hata baadhi ya kliniki zilizosajiliwa rasmi pamoja na madaktari waliohitimu hawazingatii kikamilifu taratibu na masharti ya kitaaluma.

Mnamo mwaka 2020, kisa cha mwigizaji Gao Liu kilivuma sana mitandaoni baada ya upasuaji wa pua uliomharibia sura, ambapo ncha ya pua yake ilikufa na kuwa nyeusi.

“Uso wangu ulipotea kabisa. Nilivunjika moyo mno. Taaluma yangu ya uigizaji iliangamia,” alisimulia kwa uchungu.

Upasuaji huo ulifanyika katika kliniki yenye leseni iitwayo She’s Time’s, iliyoko mjini Guangzhou, chini ya Dkt. He Ming aliyekuwa akitambulishwa kama daktari mkuu wa upasuaji na mtaalamu wa upasuaji wa pua.

Hata hivyo, uchunguzi ulibainisha kuwa Dkt. He hakuwa na sifa kamili kufanya upasuaji huo bila uangalizi, na hakuwa ameidhinishwa rasmi kuwa daktari wa upasuaji wa urembo na Tume ya Afya ya Mkoa wa Guangdong.

Mamlaka zilichukua hatua kwa kuiwekea kliniki hiyo faini, ambayo ilifungwa muda mfupi baadaye, huku Dkt. He akipigwa marufuku ya miezi sita kutekeleza majukumu ya kitabibu.

Lakini wiki chache kabla ya kufungwa rasmi kwa She’s Time’s, iliibuka kliniki mpya iitwayo Qingya ambayo iliomba kusajiliwa katika anwani ile ile.

.

Chanzo cha picha, Gao Liu

Maelezo ya picha, Operesheni isiyofaa ya mwigizaji Gao Liu – ambapo ncha ya pua yake ilibadilika kuwa nyeusi na kufa – ilienea virusi mnamo 2020.

BBC Eye imebaini uhusiano wa karibu kati ya She’s Time’s na Qingya, ikiwa ni pamoja na kutumia akaunti moja ya Weibo na kuhifadhi baadhi ya wafanyakazi wa awali, wakiwemo Dkt. He.

Aidha, taarifa zinaonesha kuwa Dkt. He alipata cheti chake rasmi cha daktari bingwa wa upasuaji wa urembo mwezi Aprili 2024, licha ya kuwa kisheria hakupaswa kuomba cheti hicho kwa kipindi cha miaka mitano tangu alipoadhibiwa mwaka 2021.

Kampuni ya Qingya sasa inadai kuwa na matawi 30 kote nchini.

Hata hivyo, Dkt. He, Qingya na Tume ya Afya ya Mkoa wa Guangdong hawakujibu maombi ya BBC ya kutoa kauli.

Kwa upande wake, Ubalozi wa China nchini Uingereza ulisema: “Serikali ya China inasisitiza kwa dhati kuwa mashirika yote yaendeleze shughuli zake kwa kuzingatia sheria, kanuni na sera husika za kitaifa.”

Miaka minne na upasuaji wa kurekebisha mara mbili baadaye, pua ya Gao Liu bado haijarejea katika hali yake ya kawaida.

“Najuta sana. Kwa nini nilikubali?” anasema kwa masikitiko.

Tume Kuu ya Afya ya China imekuwa ikijitahidi kukabiliana na tatizo la wahudumu wa afya wasio na sifa kutekeleza majukumu yanayowazidi uwezo, kwa kuchukua hatua mbalimbali ikiwemo kuagiza taasisi za afya za maeneo kuboresha udhibiti na kutoa miongozo mikali zaidi lakini bado changamoto zinaendelea kushamiri.

Kutoka kwa ofa ya kazi hadi deni na upasuaji – ndani ya saa 24

Katika China ya leo, muonekano mzuri unachukuliwa kuwa muhimu kwa mafanikio ya kitaalamu. Uchunguzi wa haraka kwenye majukwaa maarufu ya uajiri umebaini mifano mingi ambapo waajiri wanatilia mkazo mahitaji ya kimwili kwa nafasi mbalimbali za kazi, ingawa mara nyingi haya yanahusiana kidogo na majukumu halisi ya kazi. Mfano mmoja ni nafasi ya mapokezi inayohitaji wagombea kuwa “angalau 160cm mrefu na warembo,” wakati nafasi ya kazi ya utawala inasisitiza “muonekano wa kuvutia na uwepo wa kifahari.”

Hali hii inazidi kutumiwa na ulaghai unaoendelea kuongezeka katika baadhi ya kliniki za China, ambapo wanawake vijana wenye hali ya kutokuwa na kinga wanapewa ajira, lakini kwa masharti ya kulipa kwa upasuaji wa urembo wa gharama kubwa unaofanywa na waajiri wao watarajiwa.

Da Lan, jina lisilo halisi, alijaza ombi la kazi ya “mshauri wa urembo” katika kliniki moja huko Chengdu, kusini-magharibi mwa China, kupitia tovuti maarufu ya uajiri mwezi Machi 2024. Baada ya mahojiano, alipewa nafasi hiyo jioni hiyo hiyo.

Hata hivyo, anasema alipoanza kazi yake asubuhi iliyofuata, meneja wake alimuongoza kwenye chumba kidogo, alimtazama kwa makini na kisha kumwambia kuwa ili aendelee na kazi, alitakiwa kufanya upasuaji wa urembo, vinginevyo atapoteza nafasi hiyo. Da Lan anasema alipata muda wa chini ya saa moja kutafakari uamuzi wake.

Akiwa chini ya shinikizo, alikubali kufanya upasuaji wa macho mara mbili (double eyelid surgery), wenye gharama ya zaidi ya yuan 13,000 (takribani £1,330) – zaidi ya mara tatu ya mshahara wa mwezi wa kazi hiyo – pamoja na riba ya juu ya 30% kwa mwaka. Alieleza kuwa wafanyakazi walichukua simu yake na kuitumia kuomba “mkopo wa urembo,” kwa kubadilisha maelezo yake ya kipato, na ndani ya dakika moja, mkopo ulipitishwa.

Kwa saa 12, alikuwa akifanyiwa vipimo vya matibabu, na saa moja baadaye alikuwa kwenye meza ya upasuaji. Hivyo, alikua ameanza kazi, kisha akaingia katika deni kubwa na kufanyiwa upasuaji – yote hayo yakiendelea ndani ya masaa 24 tu.

Upasuaji huo haukumsaidia chochote katika matarajio yake ya kikazi. Da Lan anasema meneja wake alimdharau, akimpigia kelele hadharani na kumtusi.

Aliiacha kazi hiyo baada ya wiki chache tu. Akiangalia nyuma, anaamini kuwa kazi hiyo haikuwa ya kweli.

“Walitaka niondoke tangu mwanzoni,” anasema.

Licha ya kufanya kazi huko kwa zaidi ya siku 10, alilipwa yuan 303 tu ($42). Kwa msaada kutoka kwa marafiki zake, Da Lan alilipa deni la upasuaji wake baada ya miezi sita.

BBC Eye ilizungumza na makumi ya waathiriwa mbali na kukutana na watatu ikiwa ni pamoja na Da Lan huko Chengdu, jiji ambalo limepanga kuwa “mji mkuu wa upasuaji wa urembo” wa China.

Wengine wamenaswa katika deni kubwa zaidi kwa miaka.

Kliniki ambayo Da Lan anazungumzia limlaghai hapo awali iliripotiwa na wahitimu wengine na kufichuliwa na vyombo vya habari vya ndani, lakini bado iko wazi na bado inaajiri kwa jukumu lile lile.

Ulaghai huu hauhusiki tu kwa kazi za kliniki – unaingia katika tasnia zingine.

Baadhi ya makampuni ya utiririshaji wa moja kwa moja yanawashinikiza wanawake wachanga kuchukua mikopo kwa ajili ya upasuaji, na hivyo kuahidi umaarufu wa kuwa washawishi.

Lakini nyuma ya pazia, makampuni haya mara nyingi huwa na makubaliano ambayo hayajafichuliwa na kliniki – kuchukua fedha kutoka kwa kilamtu wanayemtuma kwenye kliniki hizo.

.

Maelezo ya picha, Katika mkahawa wa mtindo wa bohemian huko Beijing, Abby na marafiki zake wanajadili upandikizaji wa kidevu, kupunguza midomo ya juu, na upasuaji wa pua.

Katika mkahawa wa mtindo wa bohemia huko Beijing, eneo linalofaa zaidi kwa ajili ya kujipiga picha, Abby hukutana na marafiki zake ili kunywa kahawa.

Watatu hao hurekebisha mienendo yao na kubadilisha nyuso zao mbali na kope na kuunda sura mpya.

Wanapoulizwa kile wanachopenda zaidi kuhusu sura zao, wanasita, wakijitahidi kutaja sehemu moja ambayo hawangefikiria kubadilisha.

Mazungumzo yanageuka kuwa upandikizi wa kidevu, kufupisha midomo ya juu, na upasuaji wa pua.

Abby anasema anafikiria kuhusu kazi nyingine ya pua – kazi yake ya sasa ina umri wa miaka sita – lakini madaktari wa upasuaji wanaona ugumu kumfanyia upasuaji.

“Ngozi yangu hainyoosheki baada ya taratibu nyingi. Madaktari hawana kazi nyingi. Huwezi kuwapa kitambaa cha kutosha kwa vest na kutarajia mavazi ya harusi.”

Lakini licha ya hayop yote, Abby hana mpango wa kuacha.

“Sidhani kama nitaacha safari yangu ya kuwa mrembo zaidi.”