Maelezo kuhusu taarifa
- Author, Abdalla Seif Dzungu
- Nafasi, BBC Swahili
- Twitter, @SeifDzungu
- Akiripoti kutoka Nairobi Kenya
-
Dakika 30 zilizopita
Pato la Taifa (GDP) ni kiashirio kikuu kinachotumika kupima ukubwa na uwezo wa uchumi wa nchi.
Linawakilisha jumla ya thamani ya fedha ya bidhaa na huduma zote zinazozalishwa ndani ya taifa kwa muda fulani, ambao kwa kawaida ni mwaka mmoja.
Makala haya yanatoa muhtasari wa kina wa nchi 30 bora zaidi za kiuchumi barani Afrika mwaka 2025, kulingana na makadirio ya hivi punde kutoka Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF), iliyotolewa Aprili 2025.
Afrika Kusini
Kulingana na IMF, Afrika Kusini inakadiriwa kusalia kuwa nchi yenye uchumi mkubwa zaidi barani Afrika mwaka 2025 huku Pato lake la Taifa la dola bilioni 410.34, likitarajiwa kudumisha uongozi wake barani hadi angalau 2027 kulingana na repoti ya Africa View Facts.
Uchumi wa Afrika Kusini ni uchumi mchanganyiko wenye soko linaloibuka, na uchumi wa kipato cha kati, moja ya nchi nane tu za aina hiyo barani Afrika.
Uchumi wa taifa hilo ndio uchumi wa viwanda, ulioendelea zaidi kiteknolojia.
Pia unaweza kusoma
Misri
Ripoti hiyo ikinukuu IMF inasema kwamba licha ya Misri kuipiku Afrika Kusini kwa muda mfupi mwaka 2023, sasa imeshika nafasi ya pili ikiwa na dola bilioni 347.34 katika Pato la Taifa.
Misri inachukuliwa kuwa nchi yenye nguvu za kiuchumi barani Afrika hasa kutokana na Pato lake kubwa la Taifa .
Pato la Taifa la Misri ni miongoni mwa mapato ya juu zaidi barani Afrika, yakiendeshwa na sekta kama vile kilimo, utalii, mawasiliano ya simu, mauzo ya mafuta ya petroli na gesi asilia, kulingana na ISS African Futures.
Miundombinu yake ya kusafisha mafuta pia ni ya kiwango cha kimataifa, inasindika tani milioni 38 kila mwaka.
Misri pia inanufaika kutokana na eneo la kimkakati kando ya Mfereji wa Suez, ambao huwezesha biashara na uwekezaji.
Algeria na Nigeria
Algeria na Nigeria zimetinga nne bora zikiwa na $268.89 bilioni na $188.27 bilioni mtawalia.
IMF inatarajia kuwa Afrika Kusini, Misri, Algeria na Nigeria zitaendelea kutawala hali ya uchumi wa Afrika angalau hadi 2030.
Ikiwa na akiba yake kubwa ya mafuta na gesi, uwezo mkubwa katika sekta ya kilimo na utengenezaji, pamoja na sekta za huduma, na idadi ya watu inayoongezeka kwa kasi, Nigeria ina uwezekano wa kuibuka kama nchi yenye nguvu ya kiuchumi duniani.
Chanzo cha picha, Getty Images
Kenya
Jambo la kushangaza ni kwamba Kenya imeipiku Ethiopia na kuwa nchi yenye uchumi mkubwa zaidi Afrika Mashariki, ikiwa na makadirio ya Pato la Taifa la dola bilioni 131.67, ikilinganishwa na pato la Ethiopia la dola bilioni 117.46.
Nguvu ya kiuchumi ya Kenya barani Afrika inatokana na mazingira yake tulivu ya kisiasa, uchumi mseto, eneo la kimkakati, na sekta ya fedha iliyochangamka.
Mambo haya yamevutia uwekezaji mkubwa, na kuifanya kuwa kitovu cha kikanda cha fedha, uchukuzi na biashara.
Ghana
Wakati nchi kama Afrika Kusini na Misri zikiendelea kuongoza, mataifa kama Kenya, Ghana, na Tanzania yanapiga hatua kubwa, kuashiria mabadiliko makubwa katika ukuaji wa kiuchumi wa bara hilo.
Ghana inachukuliwa kuwa nchi yenye nguvu kiuchumi barani Afrika kutokana na mchanganyiko wa mambo, ikiwa ni pamoja na demokrasia yake thabiti, maliasili na uchumi imara.
Nguvu yake ni pamoja na akiba kubwa ya dhahabu, uzalishaji wa CaCao, na kuibuka kwa uzalishaji wa mafuta na gesi.
Zaidi ya hayo, eneo la kimkakati la Ghana na mazingira mazuri ya biashara huvutia wawekezaji wa kigeni
Tanzania
Tanzania inachukuliwa kuwa nchi yenye nguvu za kiuchumi barani Afrika kutokana na uchumi wake mseto, eneo lake la kimkakati, na mazingira tulivu ya kisiasa, ambayo huvutia uwekezaji kutoka nje na kuchochea ukuaji wa uchumi.
Uchumi wake mseto ni pamoja na kilimo, miundombinu, madini, na sekta ya teknolojia inayokua.
Zaidi ya hayo, nafasi ya Tanzania katika pwani ya Afrika Mashariki na demokrasia yake thabiti inachangia kuvutia wawekezaji.
Chanzo cha picha, Getty Images
Orodha ya nchi kulingana na pato la taifa
1. Afrika Kusini $410.34b
2. Egypt $347.34b
3. Algeria $268.89b
4. Nigeria $188.27b
5. Morocco $165.84b
6. Kenya $131.67b
7. Ethiopia $117.46b
8. Angola $113.34b
9. Côte d’Ivoire $94.48b
10. Ghana $88.33b
11. Tanzania $85.98b