Mwanaume mwenye umri wa miaka 72 amekamatwa na polisi nchini Ujerumani kwa tuhuma za kusababisha moto uliosababisha vifo vya watu watatu na kujeruhi wengine kadhaa katika hospitali ya Marienkrankenhaus jijini Hamburg, usiku wa Jumamosi.
Kwa mujibu wa taarifa ya polisi, mzee huyo alikuwa mgonjwa katika wodi ya wazee (geriatric ward) na alibainika kuwa mshukiwa wakati wa mahojiano na mashahidi. Polisi wamesema wanachunguza iwapo alikuwa katika hali ya msongo wa akili wakati tukio hilo lilipotokea. Anatarajiwa kufikishwa mbele ya hakimu siku ya Jumatatu.
Muuguzi wa Kijerumani avunja rekodi kwa kuuwa wagonjwa 84
Moto huo, ambao ulianza karibu saa sita usiku, ulisambaa kutoka ghorofa ya chini hadi ya kwanza ya jengo hilo la hospitali inayomilikiwa na Kanisa Katoliki. Watu watatu waliopoteza maisha walikuwa na umri wa miaka 84, 85 na 87. Watu wengine 34 walijeruhiwa, mmoja wao akiwa mahututi.
Kwa mujibu wa msemaji wa kikosi cha zima moto, kazi ya uokoaji ilikamilika ndani ya dakika 20, na watu waliokuwa ndani waliokolewa kupitia madirishani. Takriban wahudumu wa uokoaji 160 walihusika katika shughuli hiyo. Moshi ulienea katika sakafu zote nne za jengo hilo, huku wagonjwa waliokuwa kwenye majengo ya jirani pia wakichunguzwa kwa madhara ya moshi.
Hospitali yashirikiana kwa karibu na serikali kufanikisha uchunguzi
Mwandishi wa shirika la habari la dpa aliyekuwa eneo la tukio ameripoti kuwa angalau wodi moja iliteketea kabisa. Hata hivyo, maeneo ya upasuaji hayakuathirika, kwa mujibu wa msemaji wa hospitali.
Mkurugenzi mkuu wa hospitali hiyo, Christoph Schmitz, alisema kuwa taasisi hiyo inashirikiana kwa karibu na mamlaka za usalama ili kufanikisha uchunguzi. “Tumeshachukua hatua za haraka kuzuia madhara zaidi,” alisema katika taarifa.
Mdahalo kuhusu usafi wa hospitali waibuka Ujerumani
Hospitali hiyo, ambayo ni sehemu ya mtandao wa hospitali zinazomilikiwa na dayosisi ya Katoliki ya Hamburg, ni miongoni mwa hospitali kubwa zaidi za kidini kaskazini mwa Ujerumani. Ina uwezo wa vitanda 600 na huhudumia takriban wagonjwa 93,000 kila mwaka.
Askofu Mkuu wa Hamburg, Stefan Hesse, alitoa salamu za rambirambi kwa familia za waathirika na alisema: “Nina huzuni kubwa. Niko pamoja na waliofariki na waliojeruhiwa katika sala zangu.” Alisifu juhudi za vikosi vya uokoaji na kuzitaka parokia za jiji hilo kuwajumuisha waathirika katika ibada za Jumapili. Hesse alitarajiwa kutembelea hospitali hiyo.