Dec 12, 2024 04:11 UTC
Watu wenye silaha wamemuua mwanasayansi mashuhuri wa Syria mjini Damascus huku kukiwa na hofu ya kufanyika msako dhidi ya wasomi wa nchi hiyo baada ya kuondolewa madarakani serikali ya Syria hivi karibuni na makundi yenye silaha yanayoungwa mkono na mataifa ya kigeni, hasa madola ya Magharibi.
Dakta Hamdi Ismail Nadi, ambaye alikuwa amebobea katika kemia ya hali ya juu na dawa, alipatikana amekufa nyumbani kwake katika mji mkuu wa Syria siku ya Jumanne.
Taarifa zinasema kifo cha Nadi ni cha kushangaza kwani hapo awali alijulikana kama msomi wa ngazi za juu katika uwanja wake na alikuwa na michango muhimu katika utafiti wa ndani na wa kimataifa katika uga wa kemikali.
Habari ya kuuawa Dakta Nadi imeleta mshtuko katika jamii ya wanasayansi na wasomi ndani ya Syria.
Waangalizi wa mambo wamelinganisha tukio hilo na matokeo ya uvamizi wa Marekani katika nchi jirani ya Iraq mwaka 2003, ambapo baada ya uvamizi huo kulishuhudiwa kuuawa wasomi wa ngazi za juu nchini humo.
Wakati huo huo, weledi wa mambo wameonya kuhusu kupanuka wigo wa kampeni hiyo ya mauaji ya wasomi huku wakisema kuna kila dalili za kuonyesha kuhusika kwa vyombo vya kijasusi vya kigeni, likiwemo shirika la kijasusi la utawala wa Israel Mossad.
Haya yanajiri katika hali ambayo utawala haramu wa Israel umekuwa ukiripotiwa kuwa unashirikiana na wanamgambo walioiondoa madarakani serikali ya Syria siku chache zilizopita.