
Mtu mmoja aliuawa katika mji mkuu wa Kenya Nairobi siku ya Jumanne wakati wa maandamano yaliyochochewa na kifo cha mwanablogu aliyekuwa chini ya ulinzi wa polisi ambayo pia yamechochea shutuma za mauaji ya kiholela ya vikosi vya usalama. Hii ni kulingana na vyombo vya habari nchini humo .
Polisi bado haijathibitisha au kukana ripoti hiyo.
Msemaji wa polisi nchini Kenya Muchiri Nyaga alisema kuwa hakuwa na habari kuhusu majeruhi yoyote.
Maandamano haya yalifanywa kupinga kifo cha mwanablogu na mwalimu Albert Ojwang mwenye umri wa miaka 31 mnamo Juni 8 akiwa chini ya ulinzi wa polisi.
Maandamano haya yanakuja mwaka mmoja baada ya zaidi ya watu 60 kuuawa wakati wa maandamano yaliyochochewa na mapendekezo ya nyongeza ya ushuru.
Polisi walikana kuhusika
Hapo awali polisi walisema alijitoa uhai, lakini mkuu wa polisi wa Kenya aliomba msamaha baada ya uchunguzi huru kubaini kuwa majeraha ya Ojwang yaliashiria alikufa kutokana na kupigwa na na kuteswa.
Waandamanaji walipoingia barabarani katika jiji la Nairobi siku ya Jumanne, polisi walikabiliana nao kwa kuwarushia vitoa machozi.
Mapigano pia yalizuka wakati waendesha pikipiki wasiojulikana waliwapiga waandamanaji, na kuwatawanya, mwandishi wa habari wa Reuters alisema.
Kituo cha utangazaji cha NTV kilionyesha video ya waendesha baiskeli wakipiga kelele na kusema “hakuna maandamano.”
Shirika la Amnesty International ya Kenya, katika chapisho kwenye mtanfao wa X, lilielezea kuwepo kwa pikipiki zilizokuwa na abiria wawili waliojifunika kofia wakiwapiga waandamanaji na wananchi.
Rais William Ruto alisema wiki jana kuwa Ojwang aliaga dunia “mikononi mwa polisi” jambo aliloliita “kuhuzunisha moyo na halikubaliki.”
Wiki iliyopita, mamia ya watu waliandamana jijini Nairobi kuhusu kifo cha mwanablogu huyo, huku magari yakichomwa moto huku polisi wakifyatua mabomu ya machozi.
Eliud Lagat, naibu mkuu wa polisi, alisema Jumatatu alijiondoa kwa muda, akisubiri kukamilika kwa uchunguzi kuhusu kifo cha Ojwang.
Maafisa wawili wakuu na fundi wa televisheni ya mtandao (CCTV) waliokuwa wameitwa kubomoa CCTV katika kituo cha polisi, wamekamatwa kuhusiana na uchunguzi huo.