Mgogoro wa kibinadamu Gaza katika kivuli cha kuendelea jinai za utawala wa Kizayuni wa Israel

Huku zikikosoa hatua ya utawala wa Kizayuni ya kukwamisha upelekaji misaada ya kibinadamu huko Gaza, taasisi za kimataifa zimeeleza wasiwasi zilionao kutokana na kuendelea kuongezeka mgogoro wa kibinadamu katika Ukanda huo.

Mwezi wa 14 wa mauaji ya halaiki ya utawala wa Kizayuni dhidi ya watu wa Gaza unamalizika, na mashambulizi ya mabomu katika maeneo tofauti ya Ukanda huo yanaendelea huku makumi ya wakazi wa Gaza wakiuawa shahidi na kujeruhiwa kila siku. Aidha suala la njaa na maradhi limeifanya hali ya kibinadamu huko Gaza kuzidi kuzorota.

Kwa kukaribia msimu wa baridi kali, wasiwasi umeongezeka zaidi kwa sababu utawala wa Kizayuni unazuia kutumwa misaada ya kibinadamu hususan nguo za joto. Kwa kuwasili majira ya baridi, maisha yamekuwa magumu hasa kwa watu waliolazimika kuhama makazi yao na ambao wanaishi kwenye mahema.

Kanali ya habari ya Palestina “Quds” imeripoti ikinukuu vikosi vya ulinzi wa raia (vikosi vya misaada) vya Gaza kwamba: “Sambamba na kuwadia msimu wa baridi licha ya kuwa mvua ingali ndogo na nyepesi lakini katika siku hizi za mwanzo za msimu huu, mahema ya wakimbizi yameharibika kutokana na mrundikano wa maji.

Hali hii imesababisha wasiwasi wa baadhi ya mashirika ya kimataifa. Carl Skau, Naibu Mkurugenzi Mtendaji wa Mpango wa Chakula Duniani (WFP), amesema: Kamati ya Mapitio ya Njaa, ambayo ni kamati huru, ilionya kuhusu njaa iliyotabiriwa kaskazini mwa Gaza, na kusisitiza kuwa watoto katika eneo la kaskazini mwa Gaza wanakufa kwa kukosa chakula.

Image Caption

 

Akiashhiria ukweli kwamba misafara ya misaada inayoingia Ukanda wa Gaza inaporwa na utawala wa Kizayuni, Skau alisisitiza kwamba, njia za usambazaji wa misaada katika Ukanda wa Gaza lazima ziwe salama.

Hapo awali, Tess Ingram, msemaji wa Shirika la Kuhudumia Watoto la Umoja wa Mataifa (UNICEF) huko Gaza, alieleza kuwa, hali ya kaskazini mwa Ukanda wa Gaza ni ya kutisha, akisema kwamba watoto wanapoteza maisha kutokana na hali mbaya ya maisha katika Ukanda wa Gaza.

Shirika la Kutetea Haki za Binadamu la Human Rights Watch pia limetangaza kuwa, utawala wa Kizayuni unatumia uhamaji wa kulazimishwa na njaa kama silaha ya vita katika Ukanda wa Gaza. Licha ya hali mbaya ya kibinadamu kutawala huko Gaza, lakini bado utawala wa Kizayuni unaendelea kukwamisha utoaji wa misaada ya kibinadamu.

Baadhi ya vifaa vya misaada ya kibinadamu pia vinaporwa na askari na walowezi wa utawala wa Kizayuni. Hapo awali Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres akikosoa utekelezwaji wa sheria vikali na kukwamisha mambo katika zoezi la la upelekaji misaada Gaza alisema: Kuzingirwa Gaza si mgogoro unaohusiana na masuala ya kimkakati, bali ni mgogoro unaohusiana na utashi wa kisiasa na kuheshimu kanuni na misingi ya sheria za kimataifa na sheria za kibinadamu.

Jengo la Shirika la Kuhudumia Wakimbizi wa Kipalestina UNRWA likiwa limebolewa na jeshi la utawala haramu wa Israel

 

Nukta ya mwisho ni kwamba mgogoro wa Syria pia umetoa mwanya wa kushadidi jinai za utawala wa Kizayuni. Kwa sababu mtazamo wa vyombo vya habari pamoja na mtazamo wa maoni ya umma umeelekezwa kwenye mgogoro wa Syria. Utawala wa Kizayuni hivi sasa unaendelea kufanya jinai dhidi ya watu wa Gaza bila wasiwasi wowote kwani macho na masikio ya walimwengu yameelekezwa Syria.

Iwapo hakutakuweko azma na irada ya kimataifa kwa ajili ya kukomesha jinai za Wazayuni dhidi ya Gaza, basi katika miezi ijayo hali ya kibinadamu huko Gaza itaendelea kuwa mbaya na idadi kubwa ya watu wasio na hatia watapoteza maisha.