
Mashambulizi ya makombora kati ya Iran na Israel yameendelea leo kwa siku ya sitalicha ya wito wa Rais wa Marekani Donald Trump wa kutaka Iran isalimu amri bila masharti. Jeshi la Israel limesema Iran imerusha safu mbili za makombora kuelekea Israel alfajiri ya leo huku milipuko ikisikika mjini Tel Aviv. Vyombo vya habari vya Irani vimeripoti milipuko kadhaa mjini Tehran na mji wa Karaj magharibi mwa mji mkuu.
Katika taarifa yake leo, Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi wa Iran, limesema limetumia makombora ya hypersonic kuilenga Israel.
Wakati mapigano yakipamba moto, Rais Donald Trump wa Marekani ameonya kupitia ujumbe wa kwenye mitandao ya kijamii kwamba wanafahamu alikojificha kiongozi wa juu wa Iran Ayatollah Ali Khamenei, na kuongeza kuwa hawana dhamira ya kumuua angalau kwa sasa.Netanyahu: Tutashambulia kila eneo la Iran
Hayo yakijiri, wizara ya mambo ya nje ya Marekani imesema itaufunga ubalozi wake mjini Jerusalem kuanzia leo hadi Ijumaa kutokana na hali ya usalama.
Wakati huo huo masoko ya mafuta duniani yamesalia katika tahadhari kubwa, kufuatia shambulizi la kwenye kiwanda kikubwa cha uzalishaji gesi duniani kinachoendeshwa kwa ushirikiano kati ya Iran na Qatar.