Maajabu sita ya Fiston Mayele Afrika

Maajabu sita ya Fiston Mayele Afrika

By 
Charles Abel

Mwananchi Communications Limited

Muktasari:

  • Pyramids FC ni timu ya nne ya Misri kutwaa ubingwa wa Ligi ya Mabingwa Afrika ikifuata nyayo za Al Ahly, Zamalek na Ismaily.

Jumapili, Juni Mosi, 2025, mshambuliaji wa zamani wa Yanga na AS Vita Club, Fiston Mayele aliiongoza Pyramids FC ya Misri kutwaa taji la Ligi ya Mabingwa Afrika baada ya timu hiyo ya Misri kuibuka na ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini.

Katika mechi hiyo iliyochezwa kwenye Uwanja wa Juni 30, jijini Cairo Misri, Mayele alifunga bao moja huku lingine likipachikwa na Ahmed Sany wakati bao pekee la kufutia machozi la Mamelodi Sundowns lilifungwa na Iqraam Rayners.

Matokeo hayo yaliifanya Pyramids FC kutwaa ubingwa kwa ushindi wa jumla wa mabao 3-2, ikinufaika na sare ya bao 1-1 iliyopata katika mechi ya kwanza ugenini.

Kwa Fiston Mayele, ubingwa huo umekuja na heshima binafsi kwani amemaliza akiwa mfungaji bora kwa kufumania nyavu mara sita kwenye mashindano hayo msimu huu.

Kama ilivyo kwa idadi ya mabao aliyofunga, kuna mambo sita yanayoelezewa katika namba ambayo yanaonyesha namna ubingwa na mabao aliyofunga Mayele yana maana kubwa katika historia ya maisha yake ya soka.

Namba Moja

Hili ni taji la kwanza la mashindano ya klabu Afrika kwa Mayele baada ya kulikosa akiwa na klabu za AS Vita ya DR Congo na Yanga ya Tanzania.

Mshambuliaji huyo alikaribia kutwaa taji katika msimu wa 2022/2023 wakati Yanga ilipoingia katika fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika lakini taji hilo likaenda kwa USM Alger ya Algeria.

Namba Mbili

Mayele ameibuka mfungaji bora wa mashindano mawili tofauti ya klabu ya CAF kwa awamu mbili tofauti.

Msimu wa 2022/2023 alikuwa mfungaji bora wa Kombe la Shirikisho Afrika akifunga mabao saba na msimu huu amekuwa mfungaji bora wa Ligi ya Mabingwa Afrika akiwa na mabao sita.

Namba Tatu

Mayele amezifunga timu tatu tofauti za Kusini mwa Afrika katika Ligi ya Mabingwa Afrika msimu huu ambapo mbili ni za Afrika Kusini na moja ya Angola.

Timu za Afrika Kusini ambazo Mayele amezifunga ni Orlando Pirates ambayo alikutana nayo kwenye nusu fainali na Mamelodi Sundowns aliyoifunga katika fainali na ya Angola aliyoifunga ni Sagrada Esperanca.

Namba Nne

Mayele anakuwa mchezaji wa kwanza wa DR Congo kuwa mfungaji bora wa Ligi ya Mabingwa Afrika baada ya misimu minne mfululizo bila nyota wa nchi hiyo kufanya hivyo.

Kabla ya Mayele, mchezaji wa mwisho wa DR Congo kuwa mfungaji bora wa Ligi ya Mabingwa Afrika alikuwa ni Jackson Muleka aliyeibuka kinara katika msimu wa 2019/2020.

Namba Tano

Nyota huyo wa Pyramids FC anafuata nyayo za wachezaji watano tofauti wa DR Congo ambao wameibuka wafungaji bora wa Ligi ya Mabingwa wakiwa na klabu mbalimbali kuanzia 1997 wakati muundo wa mashindano hayo ulipobadilishwa.

Mwaka 2001, Kapela Mbiyavanga alikuwa mfungaji bora baada ya kupachika mabao tisa alipokuwa akiitumikia Petro Atletico ya Angola.

Tresor Mputu mwaka 2007 naye akatamba katika kufumania nyavu akiibuka kinara baada ya kufunga mabao tisa wakati akiichezea TP Mazembe.

Mwaka 2009, mfungaji bora alikuwa ni Dioko Kaluyituka wa TP Mazembe aliyepachika mabao nane na akafuatiwa na Ndombe Mubele mwaka 2014 aliyekuwa akiichezea AS Vita Club ambaye alifunga mabao sita.

Msimu wa 2019/2020, Jackson Muleka akawa mshindi kwa mabao saba na msimu huu aliyetamba ni Mayele.

Namba Sita

Mabao sita ya Mayele aliyofunga kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika ameyapata kwa kufunga katika mechi mbili ambazo kila moja alifumania nyavu mara tatu (hat trick) zote akiwa anaitumikia Yanga.

Mechi zote mbili ni dhidi ya Zalan FC ya Sudan Kusini katika msimu wa 2022/2023.

Mchezo wa kwanza Yanga ilishinda mabao 5-0 na mechi ya marudiano Yanga ikapata ushindi wa mabao 4-0.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *