Mlipuko umeharibu njia muhimu ya mitambo miwili ya nishati ya joto huko Kosovo siku ya Ijumaa, Novemba 29, na kutishia usambazaji wake wa nishati, ametangaza Waziri Mkuu wa Kosovo Albin Kurti, akilaani “shambulio” ambalo amelihusisha Serbia.

Matangazo ya kibiashara
Mlipuko wa mfereji huo, ambao hutoa maji kwa mitambo miwili ya makaa ya mawe kwa mifumo yao ya kupoeza, inayowakilisha chanzo kikuu cha umeme cha Kosovo, umetokea karibu na mji wa Zubin Potok kaskazini mwa nchi.
Ikiwa uharibifu hautarekebishwa, sehemu ya Kosovo ina hatari ya kukosa umeme mapema Jumamosi asubuhi, Waziri Mkuu amesema. “Ni jinai na shambulio la kigaidi linalolenga kuharibu miundombinu yetu muhimu,” amejibu Albin Kurti, Waziri Mkuu wa Kosovo, wakati wa mkutano na waandishi wa habari ulioitishwa Ijumaa usiku, Novemba 29, katika maoni yaliyotolewa na shirika la habari la AFP. “Shambulio hilo limefanywa na wataalamu. Tunaamini sambulio hilo limetekelezwa na magenge yanayoongozwa na Serbia,” ameongeza.
Albin Kurti hakutoa maelezo juu ya kiwango cha uharibifu uliosababishwa na mfereji huo, unaounganisha kaskazini mwa Kosovo, eneo linalokaliwa na idadi kubwa ya Waserbia, na mji mkuu wa Pristina, ambao pia hutolewa kwa sehemu ya maji ya kunywa na mfereji huu. Picha zilizochapishwa na vyombo vya habari vya ndani zinaonyesha uvunjaji upande mmoja wa mfereji ambao maji yanatoka kwa wingi.
Maoni na wasiwasi
Marekani, kupitia ubalozi wake huko Pristina,imeshutumu vikali “shambulio dhidi ya miundombinu muhimu huko Kosovo”. “Tunafuatilia hali kwa karibu […] na tumetoa msaada wetu kamili kwa serikali ya Kosovo ili kuhakikisha kwamba wale waliohusika na shambulio hili la uhalifu wanatambuliwa na kuwajibishwa,” ubalozi umesema kwenye Facebook.
Shambulio la Ijumaa linafuatia mfululizo wa matukio ya vurugu kaskazini mwa Kosovo, ambapo Waserbia ndio wengi, yakiwemo maguruneti yaliyorushwa kwenye jengo la manispaa na kituo cha polisi mapema wiki hii. Shirika la habari la AFP limejaribu kuitafuta serikali ya Serbia, ambayo haikujibu mara moja.
Mvutano kati ya Kosovo na Serbia umeendelea tangu vita kati ya vikosi vya Serbia na Kosovo mwishoni mwa miaka ya 1990. Kossovo ilitangaza uhuru wake mnamo mwaka 2008, uamuzi ambao Serbia inakataa kuutambua, na kuwahimiza Waserbia wa nchi hiyo kukataa uaminifu wao kwa Pristina.