Kenya kupambana na unyanyasaji wa kijinsia kidijitali

Wizara ya Jinsia ya Kenya imetangaza kuwa zaidi ya kesi 100 za mauaji ya wanawake zimeripotiwa katika kipindi cha miezi sita iliyopita. Nafasi ya kidijitali inaelezewa kama zana muhimu ya kujibu na kuzuia matukio haya.

Maendeleo ya kiteknolojia yamebadilisha namna jamii inavyoishi na kushughulikia changamoto mbalimbali. Mojawapo ya changamoto kubwa inayozikumba jamii nyingi duniani, ikiwemo Kenya, ni unyanyasaji wa kijinsia.

Teknolojia kusaidia katika kampeni

Ili kukabiliana na tatizo hili, serikali ya Kenya kwa kushirikiana na mashirika ya kijamii na teknolojia imeanzisha kampeni ya kidijitali dhidi ya unyanyasaji wa kijinsia, kampeni  inayolenga kutumia nguvu ya teknolojia kuelimisha, kutoa msaada kwa waathiriwa na kuhakikisha haki inapatikana kwa njia ya haraka na salama.

Kampeni hiyo imejikita katika matumizi ya majukwaa ya mitandao ya kijamii kama vile Facebook, X, na Instagram, pamoja na tovuti rasmi na programu za simu. Kupitia majukwaa haya, serikali na mashirika yanatoa elimu kuhusu aina za unyanyasaji wa kijinsia, athari zake, na hatua za kuchukua pindi mtu anaponyanyaswa. Pia, waathiriwa wanapewa fursa ya kuripoti visa vyao kupitia njia za faragha na salama, huku wakiunganishwa na huduma za ushauri nasaha, sheria, na afya.

Wasichana wa Kenya wakionyesha bangili zao baada ya kujifunza kuhusu unyanyasaji wa kijinsia
Wasichana wa Kenya wakionyesha bangili zao baada ya kujifunza kuhusu unyanyasaji wa kijinsiaPicha: Seeds of Grace

Waziri wa Jinsia, Utamaduni, Sanaa na Turathi, Hanna Cheptumo, aliyezindua rasmi Kampeni ya Kidijitali Dhidi ya Unyanyasaji wa Kijinsia nchini Kenya anasema mpango huo unalenga kukabiliana na ongezeko la kutisha la unyanyasaji dhidi ya wanawake na wasichana kupitia mbinu bunifu, zinazoendeshwa na teknolojia.

”Kampeni za kidijitali ni mojawapo ya mikakati yetu bunifu ya kuharakisha uhamasishaji dhidi ya unyanyasaji wa kijinsia ikiwa ni pamoja na mauaji ya wanawake. Kwa miezi sita iliyopita ya 2025, zaidi ya kesi 100 za mauaji ya wanawake ziliripotiwa huku nyingine nyingi zikiwa hazijaripotiwa. Unyanyasaji wa kijinsia na mauaji ya wanawake ni uhalifu mbaya ambao lazima uhukumiwe. Ni uhalifu unaohitaji uangalizi wa haraka, na hatua zinazofaa kuchukuliwa dhidi ya wahalifu,” alibainisha Waziri Cheptumo.

Magari yenye ujumbe wa kupinga ukatili wa kijinsia kuzunguka Kenya

Kupitia mpango huo, magari yenye vifaa vya kidijitali vilivyo na ujumbe dhidi ya dhuluma za kijinsia yatapelekwa katika mitaa yote ya Nairobi, yakiwasilisha ujumbe huo. Msafara huo baadaye utaelekezwa hadi miji mingine mikubwa kama sehemu ya mkakati wa kitaifa wa kuongeza ufahamu na kuhimiza mabadiliko ya tabia.

Mwezi Aprili, 2025, serikali ya Kenya iliunda jopo kazi la kiufundi kuhusu unyanyasaji wa kijinsia ambalo tayari limeanzisha vikao vya umma nchini kote. Mwenyekiti wa jopo hilo, Nancy Baraza alithibitisha kuwa wamepokea maoni mengi kutoka kwa umma, huku wengi wakishiriki kwa kusimulia hadithi za kuhuzunisha za unyanyasaji wa kimwili, kiakili na kingono.

Joan Rispa Kiragu akizungumza na wanafunzi kuhusu ukatili dhidi ya wanawake Kenya
Joan Rispa Kiragu akizungumza na wanafunzi kuhusu ukatili dhidi ya wanawake KenyaPicha: Seeds of Grace

”Kampeni ya kidijitali dhidi ya unyanyasaji wa kijinsia inalenga kufikia malengo mbalimbali. Kwanza, ni kuongeza uelewa wa jamii kuhusu unyanyasaji wa kijinsia na kuondoa unyanyapaa dhidi ya waathiriwa. Pili, ni kuhimiza watu kuripoti visa vya unyanyasaji kwa kutumia teknolojia. Tatu, ni kuimarisha mfumo wa msaada kwa waathiriwa kwa kutumia teknolojia ya kisasa. Aidha, kampeni hii inalenga kuunganisha mashirika ya serikali na yasiyo ya serikali katika mapambano dhidi ya ukatili wa kijinsia,” alisema Baraza.

Kulingana na Wizara ya Jinsia, tafiti za hivi karibuni zimefichua kuwa teknolojia inachangia pakubwa na kuongeza matukio ya unyanyasaji wa kijinsia. Utafiti uliofanywa katika vyuo vikuu na taasisi nchini Kenya ambao ulitolewa na Umoja wa Mataifa unaonyesha kuwa unyanyasaji wa kijinsia unawezeshwa sana na mitandao ya kijamii. Ripoti hiyo ilisema kuwa wanafunzi wenye umri wa kati ya miaka 20 hadi 28 wameathirika zaidi.

Soma zaidi: HRW: Wahanga wa ukatili wa kijinsia wakosa msaada Kenya

Masheki Masingila mkurugenzi mtendaji wa kituo shirikishi cha unyanyasaji wa kijinsia, aliyehusika katika utafiti huo, anasema waliohojiwa waliripoti unyanyasaji wa mtandaoni, kusambazwa kwa picha zao chafu bila idhini yao, udukuzi mtandaoni, wizi wa utambulisho wao mtandaoni, unyanyasaji wa kingono mtandaoni, watoto kuhadaiwa mtandaoni na ufikiaji usioidhinishwa wa taarifa binafsi.

Buru Abdulahi, mshirikishi mkuu wa kampeni hiyo ya kidijitali dhidi ya unyanyasaji wa kijinsia, anasema katika kukabiliana na hali hiyo, wizara ya jinsia na mashirika husika wanaazimia pia kutumia teknolojia kupambana na unyanyasaji wa kijinsia na mauaji ya wanawake. ”Tulipouanzisha mradi huu, jambo kuu lilikuwa kwamba tuweze kufikia idadi kubwa ya watu kupitia jukwaa la kidijitali. Kwa hivyo tuna matumaini kuwa ujumbe huu utawafikia wanaume na wanawake wengi zaidi katika kaunti zote,” alifafanua Buru.

Hivyo ndivyo serikali ya Kenya ilivyohakikisha inatumia teknolojia ya kisasa kupambana na unyanyasaji wa kijinsia nchini humo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *