Dec 12, 2024 06:28 UTC
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amelaani mauaji ya Khalil-ur-Rehman Haqqani, waziri wa masuala ya wakimbizi wa serikali ya kundi la Taliban nchini Afghanistan.
Ismail Baqaei amelaani vikali shambulio hilo la kigaidi lililotokea jana Jumatano mjini Kabul na kumuua waziri wa masuala ya wakimbizi wa serikali ya Taliban nchini Afghanistan Khalil-ur-Rehman Haqqani na watu wengine kadhaa.
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran pia ametoa mkono wa pole kwa familia za wahanga wa shambulio hilo la kigaidi la Daesh na kuwaombea dua za kupona haraka majeruhi wa shambulizi hilo.

Duru rasmi za serikali zimetangaza kuwa, Khalil-ur-Rehman Haqqani, Waziri wa Masuala ya Wakimbizi wa Serikali ya Taliban huko Afghanistan, ameuawa katika mripuko wa bomu ndani ya wizara hiyo.
Msemaji wa Jeshi la Polisi mjini Kabul, Khalid Zadran amethibitisha mauaji ya waziri huyo wa masuala ya wakimbizi wa serikali ya Afghanistan katika mripuko uliotokea kwenye Msikiti wa wizara hiyo jana Jumatano ambapo kundi la Taliban limesema kuwa shambulio hilo limefanywa na watu woga ambao wametoka nje ya sheria.