Dec 12, 2024 03:20 UTC
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amehutubia hadhara ya matabaka tofauti ya wananchi akigusia matukio ya hivi sasa ya Syria na eneo la Magharibi mwa Asia kwa ujumla, na kueleza sababu za kuanguka utawala wa Syria pamoja na mikakati ya Iran katika kukabiliana na hali ya sasa.
Katika kikao hicho kilichofanyika asubuhi ya jana (Jumatano), Ayatullah Ali Khamenei alisema kuwa kuanguka utawala wa Syria kumesababishwa na mambo makuu matatu:
Jambo la kwanza ni mwenendo wa utawala wa Syria wa kutotilia maanani tahadhari zilizotolewa kuhusu hali ya ndani ya nchi hiyo. Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema: “Tangu miezi kadhaa iliyopita shirika letu la upelelezi lilituma ripoti za tahadhari kwa viongozi wa Syria, sijui ikiwa ziliwafikia viongozi wakuu au zilipotea katikati. Lakini maafisa wetu wa upelelezi waliwatahadharisha katika ripoti kadha tangu miezi kadhaa iliyopita.”
Kauli hii ya Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu inaashiria kuwa, kwanza, Kambi ya Muqawama hasa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, haikushtushwa na matukio ya Syria. Pili ni kwamba, utawala wa Syria umepata hasara kubwa na kuporomoka kutokana na kupuuza tahadhari za kijasusi na kipelelezi za Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Pengine sababu ya upuuzaji huo ni ahadi hewa zilizotolewa na baadhi ya nchi za kigeni kuhusu ujenzi mpya wa Syria mkabala wa nchi hiyo kujitenga na kujiweka mbali na Iran.
Jambo la pili ni hatua za utawala wa Kizayuni wa Israel na Marekani dhidi ya utawala wa Syria. Akiashiria nafasi na mchango wa wazi wa serikali ya nchi jirani na Syria katika matukio ya sasa ya nchi hiyo, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema: “Pamoja na hayo, kuna ushahidi mwingi unaoonyesha kwamba mpanga njama na chumba kikuu cha udhibiti ni Marekani na utawala wa Kizayuni.”

Utawala wa Kizayuni wa Israel na Marekani ambazo hazikuacha kufanya jinai yoyote dhidi ya Mhimili wa Muqawama katika kipindi cha miezi 14 iliyopita, ziliendelea kushamblia utawala wa Syria sambamba na jinai zao dhidi ya Mhimili wa Muqawama. Mamia ya mashambulizi yaliyofanywa na utawala wa Kizayuni dhidi ya Syria baada ya kuanguka utawala wa Bashar al-Assad, pamoja na kukiri Marekani kwamba imefanya kwa uchache mashambulizi 75 dhidi ya Syria, ni ishara za mpango wa utawala wa Kizayuni na Marekani dhidi ya utawala wa Syria, ambao pia umeashiriwa katika hotuba ya jana ya Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu.
Sababu ya tatu ya kuanguka utawala wa Syria ni udhaifu wa jeshi la nchi hiyo dhidi ya makundi ya upinzani na ya kigaidi.
Ayatullah Khamenei amesema: “Hali ya sasa na masaibu ya Syria ni matokeo ya udhaifu na kupungua moyo wa muqawama na kusimama kidete wa jeshi la Syria.”
Jeshi la Syria, ambalo linasumbuliwa na matatizo ya kiuchumi, halikuonyesha muqawama na upinzani hata kidogo dhidi ya mashambulizi ya makundi ya kigaidi na ya upinzani, na makundi haya yalifika Damascus kutoka Idlib bila upinzani wa maana na hatimaye utawala wa Syria ulianguka katika siku 11 tu.
Kipengele kingine muhimu katika matamshi ya Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu ni kwamba, kinyume na propaganda zinazoenezwa na maadui na wapinzani, Mhimili wa Muqawama sio tu hautakuwa dhaifu mbele ya harakati za Wazayuni na Marekani, bali utaendeleza mapambano yake dhidi ya utawala wa Kizayuni na Marekani katika eneo la Asia Magharibi kwa nguvu zaidi kuliko siku za nyuma.
Kuhusiana na suala hilo, Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu amesisitiza kwamba: “Hakika vijana wenye ghera wa Syria watasimama na kukomesha hali hii kwa kusimama kidete hata ikibidi kwa kutoa mhanga, kama vijana wenye ghera wa Iraq walivyoweza kumfukuza adui kutoka kwenye nyumba zao na mitaa yao baada ya kukaliwa kwa mabavu na Marekani, kutokana na msaada na uongozi wa Shahidi wetu mpendwa. Naam, jambo hili linaweza kuchukua muda mrefu nchini Syria, lakini matokeo yake ni ya hakika.”
Suala muhimu katika matamshi ya Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu ni kwamba, madai ya kudhoofika Kambi ya Muqawama yanatokana na kutokuwa na uelewa sahihi kuhusu Muqawama na Mhimili wa Muqawama, kwa sababu “Muqawama sio kifaa kinachoweza kuanguka na kuvunjika, bali ni imani, fikra, mfumo wa kiitikadi, na uamuzi wa moyo” ambao unaimarika zaidi kwa kuwekewa mashinikizo, na ari ya watu wake inashadidi na kupata nguvu zaidi na kuenea kwenye upeo mpana zaidi kutokana na kuona maovu yanayotendeka.”