#HABARI: Watu wawili wanashikiliwa na Jeshi la Polisi mkoani Morogoro kwa tuhuma za mauaji akiwemo mmoja aliyedaiwa kumuua mtu aliyekuwa akimtuhumu kamuoa mtalaka wake na mwingine kumcharanga kwa panga baba yake mzazi.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, SACP Alex Mkama amesema tukio la kwanza limetokea Mei 26, mwaka huu katika Kijiji cha Simbalambende Kata ya Ruaha wilayani Kilosa ambapo mtuhumiwa Lucas Zacharia Kanyenze (64) mkazi wa Hyanvisi Kilosa amedaiwa kumuua mwenzake kutokana na wivu wa kimapenzi.
Kamanda huyo wa Polisi akasema mtuhumiwa Kanyenze anatuhumiwa kumuua Said Kandulu (52) mkazi wa Simbalambende kwa kumchoma kwa kitu chenye ncha kali eneo la kifuani upande wa kushoto baada ya kuibuka ugomvi wa mapenzi uliochochewa na ulevi.
Aidha, akasema mtuhumiwa mwingine Ayubu Rashid Ayubu (23) mkazi wa Gang’anda anashikiliwa na Polisi kwa tuhuma za kumuua baba yake mzazi.
SACP Mkama akasema tukio hilo limetokea Mei 29, mwaka huu majira ya asubuhi katika Kitongoji cha Gang’anda, Kijiji cha Mfuru, Kata ya Tegetero wilayani Morogoro.
Kijana huyo anadaiwa kumuua Rashid Ayubu Juma (71) mkazi wa Gang’anda kwa kumshambuliwa kwa panga maeneo ya kichwani upande wa kisogoni wakati akiwa amepumzika nyumbani kwake.
Akasema mtuhumiwa alimshambulia baba yake kisogoni mithili ya kukata mti na kusababisha kupoteza maisha na kwamba mtuhumiwa amekamatwa huku chanzo cha tukio hilo kikidaiwa ni matatizo ya Afya ya akili.
#ITVDigital #ITVUpdates #ITVTanzania.
#Follow @radioonetanzania