#HABARI: Naibu Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe

#HABARI: Naibu Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Mussa Azzan Zungu, ametoa pongezi kwa Waziri wa Maji Mhe. Jumaa Aweso pamoja na watendaji wake ndani ya Wizara kwa kutekeleza kikamilifu maelekezo ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwenye kuhakikisha kila Mtanzania anapata huduma ya maji.

Mhe. Zungu amebainisha hayo Leo Ijumaa Mei 09, 2025 wakati akihitimisha Mjadala wa Bajeti ya Wizara ya Maji kwa Mwaka 2025/26, akimtaja kama Mleta maendeleo kwenye sekta ya Maji, akikumbusha pia ‘Saluti’ aliyopatiwa na Rais Samia wakati wa uzinduzi wa Mradi wa Maji wa Same- Mwanga- Korogwe kutokana na usimamizi wa miradi ya maji nchini.

Awali, wakati wa kuwasilisha hoja yake, Waziri Aweso ameahidi kuyafanyia kazi maoni na ushauri wa Wabunge wote waliochangia kwenye Mjadala wa Bajeti ya wizara ya Maji tangu jana Alhamisi, akiahidi pia kuwajibu kwa njia ya Maandishi Wabunge wote waliochangia Bajeti hiyo kwaajili ya kutunza Kumbukumbu.

“Nitumie nafasi hii pia kwa dhati ya moyo wangu kumpongeza na kumshukuru Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, hakuna hata mmoja ambaye asiyejua, Mimi nimepata bahati ya kuwa Mbunge kwa kipindi cha miaka kumi sasa, na mimi ni Mbunge, hakuna sekta ambayo ilikuwa ya kero na lawama kama sekta ya Maji. Nitumie nafasi hii kusema dhati ya moyo, Dkt Samia Suluhu Hassan ndiyo suluhu ya matatizo ya watanzania hasa katika kumtua mama ndoo kichwani.” Amesema Waziri Aweso.

Jana Alhamisi Mei 08, 2025, Waziri wa Maji, Jumaa Aweso, aliomba Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuidhinisha jumla ya Shilingi trilioni 1.016 kwa ajili ya utekelezaji wa bajeti hiyo, ambapo asilimia kubwa ya fedha hizo zitatumika kwenye miradi ya maendeleo, bajeti ambayo tayari imepitishwa na Bunge la Tanzania.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *