#HABARI: Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi Mkoa wa Shinyanga, Jeremiah John Jilili, ametangaza kujitosa katika kinyang’anyiro cha Ubunge wa Jimbo la Solwa katika uchaguzi mkuu wa mwaka huu 2025.
Jilili amekuwa na ushawishi mkubwa katika siasa za jimbo la Solwa na mkoa wa Shinyanga kiujumla tangu mwaka 2020 alipowania ubunge kupitia mchakato wa kura za maoni ndani ya CCM, ambapo alishika nafasi ya tatu huku akiwa ndiye mgombea mwenye umri mdogo zaidi.
Mwaka 2022 alichaguliwa kuwa Mjumbe wa Kamati ya Siasa ya CCM Mkoa wa Shinyanga, na pia Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya chama hicho mkoa, nafasi ambayo anaitumikia mpaka sasa.
Katika taarifa yake aliyoitoa kwa umma, Jilili amesema, Jimbo la Solwa lina utajiri mkubwa wa rasilimali watu, madini na ardhi yenye rutuba lakini pamoja na kazi nzuri iliyofanywa na Serikali ya Chama Cha Mapinduzi bado unahitajika msukumo mkubwa zaidi wa maendeleo kutoka kwa kiongozi mwenye mbinu mpya na maono mapya.
Jilili amesema wananchi wa Jimbo la Solwa wanahitaji uhakika wa masoko ya mazao yao, ajira, miundombinu ya barabara, maji na kupanua wigo wa huduma za jamii kama afya na elimu, mambo ambayo amejipanga kuyashughulikia ipasavyo kama atapata dhamana ya kuwa Mbunge wa Jimbo hilo.