#HABARI: Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imeamuru kesi ya kuchapisha taarifa za uwongo mtandaoni inayomkabili Mwenyekiti wa CHADEMA taifa, Tundu Lissu kuendelea kusikilizwa kuanzia Mei 19, 2025 kwa njia ya Mshtakiwa kuwepo mahakamani ambapo itasikilizwa mbele ya pande zote ambapo imesisitizwa umma unakaribishwa kusikiliza kesi hiyo ila kwa kuzingatia misingi ya amani itakapokuwa inaendeshwa.
Uamuzi huo umetolewa hii leo Mei 6, 2025 na Hakimu Mfawidhi Muhini ikiwa ni baada ya hoja ambazo zililetwa na upande wa utetezi kuhusiana na kitendo cha mahakama kuamua kuendesha kesi hiyo kwa njia ya mtandao na haki ya mteja wao kusikilizwa.
Hoja za upande wa utetezi zilieleza kuwa haki ya msingi ya mteja wao kusikilizwa imekiukwa kwa kuwa sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai ambayo inataka mtuhumiwa awepo mahakamani na aweze kusikilizwa na kusaini nyaraka zinazohusika juu ya hoja zinazobishaniwa.