#HABARI: Katika kudhibiti Tembo wanaovamia na kuharibu mashamba ya wananchi wa Singida Mashariki, Serikali kupitia TAWA imesisitiza kuwa mkakati wa sasa ni kuendelea kuchukua hatua mbalimbali za udhibiti ikiwemo matumizi ya teknolojia ya ndege nyuki na kufunga visukuma mawimbi sambamba na kuweka vikosi viwili vyenye Askari 24 wakiwemo Wahifadhi 13 na Askari Wanyamapori wa Vijiji (VGS) 11 na kutoa magari matatu (3).
Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii Mhe. Dunstan Kitandula ameeleza mkakati huo wa Serikali wakati akijibu swali la Mbunge wa Singida Mashariki Mhe. Miraji Mtaturu aliyehoji juu ya mpango wa Serikali kuondoa Tembo Singida Mashariki ambao wanasumbua na kuharibu mashamba ya Wananchi.
Mheshimiwa Kitandula amesema pia wamejielekeza kuimarisha matumizi ya ndege nyuki kwa kuwafukuza tembo kutoka kwenye maeneo ya wananchi na kuwarejesha hifadhini.
Kati ya mwezi Novemba 2024 na Mei 2025, kikosi maalum cha Askari Wahifadhi 18 na VGS 6 kikitumia ndege nyuki 2 na mabomu baridi kiliweka kambi katika Jimbo la Singida Mashariki, wilayani lkungi na kufanikiwa kudhibiti makundi 23 ya Tembo kwa kuwarudisha ndani ya hifadhi.
Amesema Serikali inaendelea kutoa elimu kwa wananchi kuhusu namna ya
kuepuka madhara yanayoweza kusababishwa na wanyamapori wakali na waharibifu wakiwemo Tembo ambapo kwa kipindi cha Julai 2024 hadi Mei, 2025 elimu hiyo imetolewa kwa wananchi 517 na Askari 110 wa Jeshi la Akiba katika Kata za Mkiwa, Igombwe, lglansonia, Mangonyi, Issuna, Ntuntu na lkungi.
#ITVDigital #ITVUpdates #ITVTanzania.
#Follow @radioonetanzania