Viongozi wa Mataifa tajiri ya G7 walitatizika kuweza kusimama pamoja juu ya mzozo wa nchini Ukraine baada ya Rais Trump kuonyesha kumuunga mkono Rais wa Urusi Vladimir Putin. Trump pia aliondoka siku moja mapema kutoka kwenye mkutano huo wa kilele kwa ajili ya kuushughulikia mgogoro kati ya Israel na Iran.
Soma pia: G7 na wageni waalikwa wakutana bila Trump huku migogoro ikiwa katika ajenda kuu
Viongozi wa G7 hawakutoa tamko la pamoja la kuikosoa Urusi kwa mashambulizi yake yanayozidi kuongezeka huko nchini Ukraine. Kauli hiyo iliyopangwa ya kundi la G7 kuhusu Ukraine ilishushwa hadhi na kuwa tamko la muhtasari kutoka kwa mwenyekiti, ambaye ni waziri Mkuu wa Canada, Mark Carney, aliyetangaza mpango mpya wa vikwazo dhidi ya Urusi mara baada ya kumalizika mkutano wa kilele wa G7 siku ya Jumanne, huko Alberta nchini Canada:
Carney, alisema “Sisi pamoja na washirika wetu wa kimataifa, tumeiwekea Urusi vikwazo vipya dhidi ya watu binafsi, makampuni, meli za urusi na zile zinazopeperusha bendera ya Urusi ili kutoa shinikizo la juu kwa nchi hiyo. Wakati huo huo tumeidhinisha zaidi ya dola bilioni 2 kufadhili ndege zisizo na rubani, risasi na magari ya kivita kuisaidia Ukraine kutetea eneo lake. Pia tutaipa Ukraine mkopo wa dola bilioni 2.3 kwa ajili ya ujenzi mpya wa miundombinu ya nchi hiyo.”
Carney amesema viongozi wa G7 wanaunga mkono juhudi za Rais Trump ili kufikia amani ya kudumu nchini Ukraine na kwamba wanatambua kuwa Ukraine imejitolea kusitisha mapigano bila masharti, na wameitaka Urusi kufanya sawa na Ukraine.
Rais wa Ukraine Volodymir Zelensky, amesema amewaambia viongozi wa G7 kwamba “diplomasia sasa imetumbukia kwenye matatizo” na amewataka viongozi hao wa G7 kuendelea kumrai Rais Trump, atumie ushawishi wake kulazimisha makubaliano ya kusimamisha vita.
Wakati huo huo idadi ya vifo kutokana na shambulio la Urusi katika mji mkuu wa Ukraine, Kyiv imeongezeka. Urusi ilifanya mashambulizi hayo wakati viongozi wa kundi la la G7 wakikutana kwenye mkutamo wa kilele wa kundi hilo la nchi Tajiri Kiviwanda huko nchini Canada.
Soma pia: Viongozi wa G7 wakutana Canada
Jeshi la Ukraine limesema Urusi ilitumia ndege zisizo na rubani 440 na makombora 32 yakiwemo ya baharini kuushambulia mji wa Kyiv na kwamba vifo imeongezeka hadi watu 20. Mashambulizi hayo pia yamesababisha uharibifu wa jengo la ghorofa tisa la makaazi na taasisi za elimu.
Vyanzo: AFP/RTRE