Dec 12, 2024 06:30 UTC
Chuo Kikuu cha Al-Azhar cha nchini Misri kimelaani jinai za Wazayuni za kutumia kwao vibaya matukio ya Syria na kuteka ardhi ya nchi hiyo na kimezitaka nchi za Kiarabu na Kiislamu zichukue msimamo wa pamoja wa kuzuia kuenea donda ndugu la kensa katika Ulimwengu wa Kiarabu na Kiislamu.
Kwa mujibu wa shirika la habari la Fars, sehemu moja ya taarifa ya Chuo Kikuu cha Al-Azhar imelaani jinai za Israel za kupora na kukalia kwa mabavu ardhi nyingine za Syria pamoja na mashambulizi yake dhidi ya miundombinu na taasisi muhimu za nchi hiyo ya Kiarabu na kupora rasilimali zake.
Kwa mujibu wa gazeti la al-Quds al-Arabi, katika taarifa yake, Al-Azhar imeutaka Ulimwengu wa Kiarabu na Kiislamu kuchukua misimamo mikali na ya haraka na kutumia mashinikizo ya kimataifa ili kuzuia kuenea saratani hiyo ya Kizayuni katika mwili wa mataifa ya Kiarabu na Kiislamu na kwengineko.
Chuo hicho kikuu cha Kiislamu cha Misri vilevile kimesema kwamba kinafuatilia kwa karibu matukio ya Syria na kinawataka wananchi wa nchi hiyo waelewe umuhimu wa kushikamana na kulinda haki ya kujitawala ardhi yote ya nchi yao.
Aidha kimewaonya Wasyria wote wasiwe tayari kutumiwa kufanikisha njama hatari za kuimega vipandevipande nchi yao na kutumbukizwa kwenye tope na kinamasi cha migogoro na vita vya wenyewe kwa wenyewe.
Al Azhar pia imesisitiza kuwa, baadhi ya madola maovu hayataki Syria iwe na utulivu na ustawi na imetaka wananchi wa nchi hiyo kuwa waangalifu na kutopuuza hata chembe hali tata ya nchi yao na eneo hili kiujumla.