Afrika Kusini yahimiza kutatuliwa kero za usafi katika mpaka wake na Msumbiji

 

Dec 12, 2024 06:28 UTC

Bunge la Afrika Kusini limehimiza kuweko ushirikiano kati ya mamlaka husika za nchi mbili ili kushughulikia kero zinazoendelea kujitokeza kwenye huduma za mpaka wa nchi hiyo na Msumbiji.

Uhimizaji huo umekuja baada ya Mamlaka ya Usimamiaji wa Mipaka ya Afrika Kusini (BMA) kusimamisha kwa muda shughuli za eneo la mpakani la Lebombo Jumatatu wiki hii kutokana na maandamano yanayohusiana na uchaguzi wa Msumbiji yaliyotokea karibu na mpaka wa Afrika Kusini. Kivuko hicho kimekuwa kikifungwa mara kwa mara tangu baada ya kutangazwa matokeo ya uchaguzi nchini Msumbiji Oktoba 24, 2024.

Chama cha Usafirishaji Mizigo cha Afrika Kusini (RFA) kilisema Jumanne kwamba kusimamishwa shughuli za kivuko cha Lebombo kunasababisha hasara ya takriban randi milioni 10 (kama dola za 562,400 za Kimarekani) kila siku.

Msururu wa magari ya mizigo yaliyokwamba kwenye mpaka wa Msumbiji na Afrika Kusini kutokana na maandamano ya baada ya uchaguzi ya nchini Msumbiji

 

Vyombo vya habari vimeripoti kuwa, waandamanaji upande wa Msumbiji wamefunga njia muhimu ambayo kwa kawaida hutumiwa na zaidi ya malori 1,000 yanayosafiri kila siku kuelekea Bandari ya Maputo. Kufungwa kwa muda njia hiyo kunasababisha kukatika huduma na kuchelewa kufika bidhaa na abiria. Hivi sasa kunashuhudiwa msururu mrefu wa malori yanayosubiri kuingia Msumbiji.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, kamati ya Bunge la Afrika Kusini imemaliza ziara yake ya kukagua eneo hilo na kubainisha wasiwasi wake kuhusu athari za kuchelewa kwa muda mrefu uvuushaji bidhaa mpakani kutokana na maandamano ya nchini Msumbiji. 

Katika tamko lake, kamati hiyo ya Bunge la Afrika Kusini imesema: “Ushirikiano endelevu ni muhimu kati ya serikali ya Afrika Kusini na Msumbiji ili kupata masuluhisho ya changamoto za hivi sasa.”