SHIRIKISHO la Soka Zanzibar (ZFF), limeipiga faini ya Sh3 milioni, KVZ baada ya kubainika mashabiki wake kufanya vurugu katika mechi ya nusu fainali ya Kombe la Shirikisho (ZFF Cup) dhidi ya Uhamiaji.
Mechi hiyo iliyochezwa Juni 11, 2025 saa 10 jioni kwenye Uwanja wa Mao A, kisiwani Unguja, KVZ ilitoka na ushindi wa mabao 2-1 na kufuzu hatua ya fainali ya michuano hiyo ambapo jioni ya leo itashuka uwanjani kuvaana na KMKM.
Taarifa iliyotolewa na Katibu wa Kamati ya Mashindano ya ZFF, Ali Bakar Ali ‘Cheupe’, imeeleza shirikisho hilo limepitia ripoti ya mwamuzi, kamisaa, mratibu wa mechi na maelezo kutoka kwa ofisa wa ulinzi na usalama kuhusiana na fujo zilizojitokeza katika mchezo huo.
Taarifa hiyo imeeleza kwamba baada ya mchezo huo kumalizika iliripotiwa kuwa baadhi ya mashabiki na wachezaji wa Uhamiaji waliwafuata waamuzi na kuwatolea maneno ambapo Steward walifika na kuwatoa nje.
Wakati Sterward wakifanya hivyo, ghafla mashabiki na askari wa KVZ waliingia uwanjani wakiwa wameficha sura zao wakiwa na silaha na kuwashambulia wachezaji na viongozi wa benchi la ufundi.
Kufuatia ripoti ya wasimamizi wa mchezo na baadhi ya picha za matukio zilizotumwa kwenye mitandao ya kijamii kuhusiana na kadhia hiyo, Kamati ya Mashindano ZFF imefikia uamuzi wa kuitoza KVZ faini ya Sh3 milioni ambazo zinatakiwa kulipwa kabla ya mchezo wa fainali utakaochezwa Juni 22 mwaka huu.
“Adhabu hii ni kwa mujibu wa sura ya ishirini (3) (ii&iii) ya Kanuni ya Mashindano ZFF 2024-2025. Kwenda kinyume cha agizo hili kutaiwezesha Kamati ya Mashindano kutoa adhabu zaidi kwa mujibu wa Kanuni ya Mashindano inavyoelekeza,” ilisema taarifa hiyo.
Kamati hiyo pia imetoa onyo kali kwa kiongozi wa Uhamiaji FC, Mwinyi Hamad ambaye kama atarudia kufanya makosa hayo ZFF itamchukulia hatua kama Kanuni ya Mashindano inavyoelekeza sura ya ishirini (3) (i).
Katika hatua nyingine, Kamati ya Waamuzi ya ZFF imemfungia kwa miezi mitatu mwamuzi Thobias Warriko aliyecheza pambano hilo la nusu fainali ya FA kwa kushindwa kutafsiri sheria za soka.
Juni 12, 2025, Klabu ya Uhamiaji ilitoa taarifa ikisema wachezaji wao saba na baadhi ya viongozi wa benchi la ufundi waliumizwa vibaya katika vurugu hizo na waliripotiwa kituo cha Polisi Madema na kupewa PF3 kwa hatua za matibabu.