Rais Donald Trump amesema kwamba Marekani inafahamu alikojificha Kiongozi wa juu zaidi wa Iran Ayatollah Ali Khamenei katika kipindi hiki cha mzozo kati ya Israel na Iran, lakini hataki auawawe kwa sasa. Katika ujumbe wake aliouchapisha kupitia mitandao ya kijamii, Trump ameitaka Iran “kusalimu amri bila masharti” huku mzozo huo ukizidi kuongezeka.
“Tunajua haswa ni wapi huyo anayeitwa ‘Kiongozi Mkuu’ alikojificha. Ni rahisi kumpata lakini yuko salama huko aliko, hatutomuua angalau kwa sasa,” aliongeza Trump katika chapisho lake.
Matamshi ya Trump yanayozidi kuwa makali kwa serikali ya Iran ameyatoa baada ya kuwahimiza wakaazi zaidi ya milioni 9 wa Tehran kuondoka ili kuokoa maisha yao huku akikatiza ushiriki wake katika mkutano wa kilele wa nchi saba tajiri kiviwanda za G7 na kurejea Washington kwa mazungumzo ya haraka na washauri wake wa kiusalama. Hapo awali, Trump alichapisha ujumbe mwingine akitangaza juu ya udhibiti kamili wa anga ya Tehran.
Mapigano yaingia siku ya sita
Mashambulizi baina ya nchi hizo mbili yameendelea yakiingia siku ya sita. Iran kwa mara nyingine imefyatua mkururo wa makombora kuelekea Israelhuku nchi hiyo nayo ikiushambulia mji mkuu Tehran na miji mingine ya Iran. Hadi kufikia sasa, watu waliouawa nchini Israel ni 24 na zaidi ya 600 kujeruhiwa. Na huko nchini Iran watu zaidi ya 200 wameuawa.
Wakati huo huo jeshi la ulinzi la Israel IDF limeripoti mapema asubuhi ya leo kwamba makombora zaidi kutoka Iran yanazidi kufyatuliwa. Vingora vya tahadhari vilisikika huku jeshi la Israel likiwahimiza raia wake kufuata maelekezo yanayotolewa na idara ya tahadhari ya IDF.Netanyahu asema watasambaratisha viongozi wa usalama wa Iran
Ripoti hiyo inafuatia onyo lililotolewa na mkuu wa utumishi wa jeshi la Iran, aliyewataka watu kuondoka katika miji mikubwa ya Israel ya Tel Aviv na Haifa. Wakaazi wa mji mkuu wa Iran walionekana pia wakiondoka mjini huku maduka na masoko ya kihistoria mjini Tehran yakifungwa Jumanne.
Urusi na China zatoa tamko
Rais wa China Xi Jinping ameelezea ‘wasiwasi wake mkubwa’ juu ya kuongezeka kwa mvutano kati ya Israel na Iran na kusema kwamba serikali ya Beijing inaweza kusaidia katika juhudi za kurejesha amani na utulivu katika eneo hilo.
Na Urusi iliyo mshirika wa Iran, imeishutumu Israel kwa kuuelekeza ulimwengu katika janga la nyuklia kufuatia kuongezeka kwa machafuko kanda ya Mashariki ya Kati.China yawarai raia wake nchini israel kuondoka haraka
Urusi imeitaka Israel kusitisha mashambulizi yake kwenye vituo hivyo vya nyuklia na maeneo yanayofuatiliwa na Shirika la Kimataifa la kudhibiti nguvu za Atomiki.