
Waziri wa Mambo ya Nje wa Uturuki Hakan Fidan na mwenzake wa Urusi Sergey Lavrov Jumapili wamejadiliana kuhusu mgogoro unaoendelea kati ya Israel na Iran.
Katika mazungumzo kwa njia ya simu, viongozi hao pia wamejadiliana uwezekano wa athari za kikanda na kidunia kufuatia kuongezeka kwa hali ya wasiwasi, kwa mujibu wa vyanzo vya kidiplomasia.
Akionyesha wasiwasi kuhusu hali inavyoendelea, Fidan amesisitiza kwamba diplomasia ndio njia pekee ya kumaliza uhasama na kutatua migogoro inayohusu mipango ya nyuklia ya Iran.
Israel ilianzisha mashambulizi ya anga katika maeneo mbalimbali nchini Iran, ikiwemo maeneo ya kijeshi na nyuklia, mwanzoni mwa Ijumaa, na kuifanya Tehran kujibu mashambulizi ndani ya saa kadhaa.
Serikali ya Israel imesema kwamba takriban watu 13 wameuawa na zaidi ya 370 kujeruhiswa kufuatia mashambulizi ya anga ya Iran tangu Ijumaa.
Iran kwa upande wake, imesema kwamba, watu 78 wameuawa siku ya kwanza ya mashambulizi ya Israel, na wengine zaidi, ikiwemo watoto, waliuawa siku ya pili.