Uwezo wa kiongozi wa kidini wa Iran Ayatollah Ali Khamenei

Ayatollah Ali Hosseini Khamenei ndiyo mkuu wa nchi, amiri jeshi mkuu na ndiyo mwenye kauli ya mwisho inapotokea suala la amri, maagizo na sera za nchi katika masuala mbalimbali.

Kiongozi wa kidini wa Iran ana uwezo na ushawishi juu ya mihimili ya serikali, bunge na mahakama. Wagombea wote wa urais na nafasi za juu za uchaguzi wanafanyiwa mchujo na baraza la wanazuoni 12, ambao hao wanazuoni wanateuliwa moja kwa moja na kiongozi huyo wa kidini.

Aliyeko kwenye nafasi hiyo kwa sasa ni Ali Hosseini Khamenei ambaye alichukuwa wadhifa huo mwaka 1989 baada ya kifo cha Ruhollah Musavi Khomeini.

Ali Hosseini ni kiongozi wa pili wa kidini wa Iran na amekuwepo kwenye nafasi hiyo kwa zaidi ya miaka 35 kufikia sasa akiwa ndiye kiongozi aliyehudumu kwa muda mrefu zaidi.

Kabla ya kuwa kiongozi wa nchi, aliwahi kuwa rais wa nchi hiyo kati ya mwaka 1981 na 1989. Kwa hiyo kupata kwake wadhifa wa kuongoza nchi, Khamenei inaaminika kuwa alikuwa tayari amependekezwa na Khomeini kumrithi katika nafasi hiyo.

Nafasi yake haipitii katika mchakato wa uchaguzi, lakini mwanasiasa yoyote haingii katika uchaguzi bila yeye na jopo lake kukupiga msasa na kukupa ridhaa.

Na inapokuja suala la kufanya maamuzi ambayo ni magumu na yenye athari kubwa kwa nchi, ndipo sauti ya Khamenei husikika kama ilivyo kwa vita kati ya Israeli na Iran.

Labda ni kutokana na ushawishi huo na nafasi yake ya kisiasa nchini Iran, ndio Rais wa Marekani Trump anaripotiwa kutounga mkono wazo la Israeli la kutaka kumuua kiongozi huyo.

Hata hivyo, kumekuwa na jaribo la kutaka kumuua katika miaka ya nyuma ambapo alinusurika, lakini kusababisha mkono wake wa kulia kupooza.
Kiongozi huyo wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ana umri wa miaka 86.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *