Ukraine yapokea miili zaidi ya 6,000 ya wanajeshi wake

Ukraine imepokea miili miengine 1,245 ya wanajeshi wake waliouawa vitani na Urusi, hatua ya mwisho katika makubaliano ya kurejesha maiti zaidi ya 6,000 yaliyofikiwa kwenye mazungumzo ya amani mjini Istanbul mapema mwezi huu.

Kwa mujibu wa Waziri wa Ulinzi wa Ukraine, Rustem Umerov, jumla ya miili 6,057 imeshapokelewa hadi sasa, huku Urusi ikisema imekabidhi jumla ya maiti 6,060 — tofauti ndogo ya takwimu ambayo haijafafanuliwa rasmi.

Kwa upande wake, Urusi imesema iko tayari kukabidhi maiti nyingine 2,239 za wanajeshi wa Ukraine, nje ya makubaliano ya awali. Hii inaifanya kuwa moja ya operesheni kubwa zaidi za urejeshaji wa miili tangu uvamizi wa Urusi kuanza mwaka 2022.

Urusi, kwa upande wake, imepokea maiti 78 za wanajeshi wao waliouawa katika mchakato huu. Hata hivyo, tofauti na Ukraine, Urusi haikuonyesha mpango wa kuongeza idadi hiyo kwa sasa.

Katika ujumbe wa mitandao ya kijamii, Waziri Umerov amesema Ukraine haitasimama: “Tunasonga mbele sasa kwa hatua inayofuata — kurejesha wafungwa wa vita,” alisema waziri huyo.

“Tunaendelea kuwafurusha Warusi”

Wanajeshi wa Ukraine baada ya zoezi la kubadilishana wafungwa kati ya Urusi na Ukraine
Wanajeshi wa Ukraine baada ya zoezi la kubadilishana wafungwa kati ya Urusi na UkrainePicha: Ukrainian Presidential Press Service/Handout/AFP

Mabadilishano haya ya maiti na wafungwa ndio mafanikio pekee yaliyoonekana kwenye mazungumzo kati ya Kyiv na Moscow yaliyofanyika Istanbul. Hakukuwa na makubaliano ya kusitisha vita, wala ramani ya amani ya muda mrefu.

Sambamba na hayo, Rais Volodymyr Zelenskiy alitangaza kuwa jeshi la Ukraine limekomboa kijiji cha Andriivka katika mkoa wa Sumy, pamoja na mafanikio mengine mashariki mwa nchi, kama vile maeneo ya Pokrovsk na Kupiansk.

“Kamanda Mkuu Oleksandr Syrskyi ameripoti kuhusu mstari wa mbele. Tumetoa msisitizo maalum kwa eneo la Pokrovsk na maeneo ya mpaka wa Sumy. Tunaendelea kuwafurusha Warusi, na nawapongeza wanajeshi wote wanaoleta matokeo haya”, alisema Zelensky.

Zelenskiy ameitembelea Austria leo, ikiwa ni ziara yake ya kwanza nchini humo tangu uvamizi wa Urusi kuanza. Alikutana na Rais wa Austria Alexander Van der Bellen na Kansela Christian Stocker kujadili amani, huku wake zao wakiongoza mjadala wa ushiriki wa wanawake katika kujenga usalama wa kimataifa.

Wakati Austria ikiendelea kushikilia msimamo wa kutoegemea upande wowote, nchi hiyo imekumbwa na ukosoaji mkubwa kwa kuendeleza uhusiano wa kidiplomasia na Moscow. Huku mchakato wa mazungumzo ukiwa bado unasuasua, hali ya hatari inaendelea kushuhudiwa, hasa baada ya Urusi kurusha droni 138 za mashambulizi usiku kucha nchini Ukraine.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *