Rais wa Marekani Donald Trump amesema anatafuta suluhisho la kweli kwa mzozo wa nyuklia na Iran na ameashiria kuwa anaweza kuwatuma maafisa waandamizi – akiwemo mjumbe wake Steve Witkoff au Makamu wa Rais JD Vance – kwa mazungumzo na Tehran. Akizungumza baada ya kuondoka mapema kwenye mkutano wa G7 nchini Canada, Trump alikanusha kuwa hatua hiyo ilikuwa ya kutafuta usitishaji mapigano, akisema kuna jambo “kubwa zaidi” linaendelea.
Katika muktadha huo huo, Waziri wa Ulinzi wa Israel, Israel Katz, alitoa onyo kali kwa Kiongozi Mkuu wa Iran Ayatollah Ali Khamenei, akisema anaweza kufuata mkondo kama wa Saddam Hussein wa Iraq. Saa chache baadaye, milipuko ilisikika mjini Tehran na Isfahan, ikiripotiwa na vyombo vya habari vya Iran. Huku hayo yakijiri, Trump alitabiri kuwa Israel haitapunguza kasi ya mashambulizi dhidi ya Iran.
Waziri Mkuu wa Uingereza Keir Starmer alisema kuwa Trump hajatoa ishara yoyote kuwa Marekani iko tayari kujiingiza moja kwa moja katika vita kati ya Israel na Iran. Tamko la G7 liliunga mkono Israel lakini pia liliitaka pande zote kupunguza mvutano, huku Merz wa Ujerumani akisema Israel inafanya “kazi chafu kwa niaba ya wote.” Merz aliongeza kuwa iwapo Iran haitarejea mezani kwa mazungumzo, uharibifu kamili wa program ya nyuklia ya Tehran unaweza kuzingatiwa kwa msaada wa Marekani.
Wakati huo huo, Rais Trump alitoa wito kwa wakaazi wa Tehran kuhama mara moja kupitia ujumbe mkali aliouchapisha kwenye Truth Social. Hii ilijiri huku Israel ikiendeleza mashambulizi makubwa dhidi ya maeneo ya kijeshi na nyuklia ya Iran, yaliyosababisha vifo vya watu 244 na majeruhi 1,277, wengi wao wakiwa raia. Iran ilijibu kwa mashambulizi ya makombora na droni, na kuua zaidi ya raia 20 wa Israel.
Mahujaji wa Iran wakwama Iraq wakihofia usalama wa familia zao
Zaidi ya Wairani 400 waliovuka mpaka kutoka Saudi Arabia hadi Iraq baada ya Hija, wamekwama mjini Ayn Tamr huku wakiwa na wasiwasi mkubwa kuhusu familia zao. Baadhi walilia kwa uchungu walipopokea taarifa za vifo na kutoweka kwa wapendwa wao kutokana na mashambulizi ya Israel dhidi ya Tehran. Wanawake wengi walieleza hofu kuhusu hali ya watoto wao, huku wengine wakifurahia kuwasiliana kwa mara ya kwanza baada ya siku kadhaa.
Serikali ya Iraq inatarajiwa kuwapokea mahujaji wa Iran wapatao 76,000 waliokwama kutokana na kufungwa kwa viwanja vya ndege vya Saudi Arabia. Kila siku, Wairani 2,500 wanapangwa kusafirishwa kupitia mpaka wa Mehran ili kurudi nyumbani kwao.
Miongoni mwao ni Aziz Yussef, ambaye alisikia mlipuko ulitokea kilomita moja kutoka nyumbani kwake mjini Kermanshah akiwa bado Saudi Arabia. Alieleza hofu yake akisema, “Wameleta vita nyumbani kwetu. Hawapigani sisi tu, bali pia Gaza na Syria – na Marekani haiwazuii.”
Yussef na mkewe hutumia kila fursa ya kupata intaneti kufuatilia taarifa kupitia simu na runinga, wakitumaini kupata habari njema kuhusu usalama wa familia zao. Japokuwa ana matumaini ya kurudi Iran, bado hajui atafika vipi nyumbani kwake kutokana na hali ya sintofahamu iliyoikumba nchi hiyo.
Chanzo: Mashirika