WAKATI Kaizer Chiefs ya Afrika Kusini ikiendelea na mazungumzo ya kuhitaji huduma ya mshambuliaji wa Simba, Steven Mukwala, inaelezwa RS Berkane imeingilia kati dili hilo kwa kuweka dau nono ili kumchomoa nyota huyo kutoka kwenye viunga vya Msimbazi.
Hadi kufikia hatua ya kuhitaji kumsajili Mukwala, inaelezwa RS Berkane ilivutiwa na kiwango alichokionyesha mshambuliaji huyo katika fainali ya pili ya Kombe la Shirikisho Afrika iliyochezwa Mei 25 mwaka huu kwenye Uwanja wa New Amaan Complex, Zanzibar na kumalizika kwa sare ya 1-1, kisha Simba ikapoteza kwa jumla ya mabao 3-1 kufuatia ugenini kufungwa 2-0.
Katika mchezo huo ambao Mukwala alicheza dakika zote tisini baada ya ule wa kwanza ugenini kuishia benchini, alifunga bao lakini lilikataliwa baada ya mapitio ya VAR kubaini alikuwa ameotea kabla hajauweka mpira nyavuni kwa kichwa.
Imeelezwa uongozi wa RS Berkane umeweka dola 300,000 (takribani Sh791.6 milioni za Kitanzania) ili kuishawishi Simba kuvunja mkataba wa miaka miwili iliyobaki kwa mshambuliaji huyo raia wa Uganda aliyetua hapo mwanzoni mwa msimu huu akitokea Asante Kotoko ya Ghana.
Mukawala ambaye wakati anatua Simba iliripotiwa amesaini mkataba wa miaka mitatu, tayari ametumikia mwaka mmoja unaokwenda kumalizika mwishoni mwa msimu huu akiwa amefunga mabao 12 na asisti tatu kwenye Ligi Kuu Bara.
“Simba ina ofa hizo mbili mezani na timu mojawapo ikifanikiwa kununua mkataba uliobaki basi uongozi utaingia sokoni kusaka mshambuliaji mpya wa kigeni,” kilieleza chanzo hicho na kuendelea:
“Mukwala alisajiliwa na Simba kwa mkataba wa miaka mitatu, tayari ametumikia mmoja, imebaki miwili na akiuzwa kutakuwa na uwezekano wa kumbakiza Leonel Ateba ambaye jina lake lipo katika orodha ya wachezaji ambao wanaweza kuondolewa.”
Chanzo hicho kilisema hivi karibuni uongozi wa Kaizer Chiefs, Simba na wanaomsimamia Mukwala walifanya mazungumzo kuhusu ofa ya mchezaji huyo likiwa ni pendekezo la kocha Nasreddine Nabi aliyewahi kuinoa Yanga kuanzia 2021 hadi 2023.
Mchezaji mwingine ambaye Nabi alimpendekeza asajiliwe katika kikosi cha Kaizer Chiefs ni Feisal Salum ‘Fei Toto’ wa Azam FC anayeongoza kwa asisti 13 akifunga mabao 4.