#HABARI: Hospitali ya kisasa na kituo cha umahiri wa matibabu Barani Afrika, itasaidia kubadilishana ujuzi wa kitabibu, kutoa mafunzo kwa wataalamu na kuendeleza utafiti katika magonjwa ya saratani, moyo na maeneo mengine muhimu ya tiba ili kuboresha huduma hizo nchini Tanzania.
Waziri wa Afya Mhe. Jenista Mhagama amesema hayo leo, akimwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan, wakati akiwa katika uzinduzi wa awamu wa kwanza ya Hospitali ya kisasa na kituo cha umahiri wa matibabu Barani Afrika kilichojengwa Jijini Abuja Nigeria.
“Kituo hiki cha Umahiri wa Tiba (AMCE) si tu mafanikio ya Kitaifa kwa Nigeria bali ni matumaini, ubunifu na ustahimilivu kwa sekta ya afya barani Afrika ikiwemo Tanzania kwa kuwakilisha maono yetu ya pamoja ya Kiafrika ya kujitegemea, kuimarisha ushirikiano wa kikanda na kuimarisha mifumo ya afya sambamba na ajenda 2063,” Amesema Waziri Mhagama
Waziri Mhagama amesema Tanzania itaendelea kushirikiana na Nigeria katika sekta ya afya kwa kuwa Afrika inakua imara zaidi wakiendelea kushirikiana, AMCE litawahudumia si tu wananchi wa Nigeria bali pia wagonjwa kutoka pembe zote za Afrika ikiwemo Tanzania.
“Naipongeza Serikali ya Shirikisho la Nigeria, AFREXIMBANK, King’s College London, na wadau wote kwa uwekezaji huu mkubwa wa dola za Marekani milioni 300, hii iwe ni chachu ya kuanzishwa kwa miradi kama hii sehemu nyingine za Afrika,” Amesema Waziri Mhagama
#ITVDigital #ITVUpdates #ITVTanzania.
#Follow @radioonetanzania